.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Mvuvi

 

 

 

 

 

 

Related links

 

Mvuvi

31 March, 2002

  1. Ndimi mvuvi halisi, kula vuvi nalijuwa
    Nivuwaye mikambisi, na papa wenye khatuwa
    Wala sivui vingisi, mishipi haisumbuwa
         Nimekwambiya elewa

  2. Sivuwi bahari ndogo,hatia nanga fuoni
    Havisimbika vigogo, vilivyozama majini
    Na wala sivuwi ngogo, vidagaa na mbinini
         Siwavui asilani

  3. Jabali hulijilisi, jishipi nikalitupa
    Haotea mifulusi, na nguru na mijipapa
    Si kasikazi si kusi, khabari yangu nakupa
         Wala sivui kwa pupa

  4. Na nivuapo malema, huingia ndani ndani
    Maji yangu ni ya pima, thalatha u thalathini
    Na ndiyo ninayozama, lema halibwaga tini
          Uliza mimi n'nani?

  5. Na nivuapo maziyo, mavuvi ya kizamani
    Kwa hino hali niliyo, huvua kwa kutamani
    Hatafuta kiteweyo, cha wali mwema kombeni
          Haandaa siniani

  6. Ela uvuvi wa juya, kuvua siutamani
    Sababuye takwambiya, ufahamiwe mwendani
    Ni kwambakwe huingiya, samaki waso thamani
          Kama wewe mwafulani

  7. Ni kuu yangu bahari, elewa sana elewa
    Huko hakwendi Vihori, wala vyenu vimashuwa
    Shoti nakhodha hodari, kisha ende kwa ngalawa
          Na milango kuijuwa

Kutoka Malenga wa Mvita

Limeletwa na Maher Fundi


Mvuvi

03 April, 02

  1. Shairi limesukika, mjuzi hatosumbuka
    Mvuvi wa kusifika, avua anapotaka
    Havui vitakataka, samaki anayetaka.

  2. Kofia nakuvulia, na koja ninakuvika
    Vibua waviachia, dagaa mwiko kushika
    Simvuvi sinzia, ndio maana unawika.

  3. Beti tatu nachangia, kukupa heko sawia
    Wengine wamo kulia, mbinu unazotumia
    Waloweze kuwambia, nyayo zako kufatia.

wakatabahu

Hashil S. Hashil


Mvuvi

  1. Mvuvi na zako hila, kujisifu si wosia.
    Mvuvi wacha papara, bahari si yako ndia.
    Mvuvi unaokula, ni samaki wa bandia.
    Nakwambia hujavua.

  2. Mvuvi huna haraka, kwa samaki walolala.
    Mvuvi zamia sana, bahari za vina saba.
    Mvuvi wavua koa, kwa huko hakuna kamba.
    Hawana ladha wa huko.

  3. Mvuvi yako bahari, na milango kuijua.
    Mvuvi yako nadhari, samaki kuwachagua.
    Mvuvi huna habari, wengine si wakuliwa.
    Wapevu wanuka vumba.

Walii Genderi.


Mvuvi


Date: 11 Apr 2002

  1. Mvuvi kutaharuki, Kwenye maji ufukweni
    Mishipi haishikiki, Chambo hakionekani
    Imekufika hilaki, Mvuvi wavua nini
  2. Tambua hao samaki, Waishio baharini
    Kuna dhofu walo dhiki, Wajao hata demani
    Lakini kuna malaki, Kwao chambo si thamani
  3. Mvuvi zako hamaki, Na maguvu muilini
    Watwambia hawatoki, Watulia na yamini
    Mbona kutahamaki, Wameshapenya nyavuni
  4. Nakwambia usadiki, Uvuvi pia ni fani
    Ujifunze umiliki, Maarifa kubaini
    Kwanini huambiliki, Samaki hawi mwambani
  5. Nisikize sidhihaki, Tutaonana mwakani
    Papa chambo hakitaki, Aja mwenyewe chomboni
    Kuvua kipande hiki, Wajisifu bandarini

A. Baja

Mvuvi


  1. Yarabi salama, leo ishapita.
    Na jua lazama, tamaa nakata.
    Mechoka tazama, macho yafukuta.
       Mbona hajarudi,mvuvi matata.

  2. Sasa wiki moja, hajatuzukia.
    Katoka kwa hoja, kwenda tuvulia.
    Samaki wa haja, anaojilia.
       Mbona hajarudi.

  3. Twemwambia zama, samaki si hao.
    Watakuangama, vumba ndio lao.
    Mbona hakuvuma, kwa kuwala hao.
       Kenda vua wapi.

  4. Vihori havyendi, huko avuako
    Nasi hatufiki, bahari za vumo.
    Kina sikiwezi, nikaduru humo.
       Mwenzetu kazama.

  5. Mpandao meli, tazameni huko.
    Mvuvi habari, nyumbani hayupo.
    Yu kwenye hatari, humo avuamo.
       Bahari si lake shamba.

Walii Genderi.

N-GONGELE


Mvuvi


  1. Walii genderi, tua roho yako
    Mvuvi mahiri, bado yungaliko
    Ana yake siri, kwa huko aliko
    atarudi papo

  2. Ilikuwa kali, dharuba ya kusi
    Ikangia vuli, hana wasiwasi
    Alivua kweli, mapapa na ngisi
    Poa roho basi

  3. Tarudi nyumbani, na mavuvi tele
    Tena salimini, punguza kelele
    Miye naamini, ana lake yule
    Mso hili ana lile

  4. Siku ikifika, nitakukumbusha
    Tena kwa hakika, nitakuamsha
    Mvuvi kafika, tena kwa bashasha
    Nyavu karejesha

Mbarouk

N.York


Mvuvi


28 April, 2002

        Sie mvuvi wa pweza

  1. Mwenye kutaka kujuwa, huenda kwenye kiini
    Ili apate elewa, kimekusudiwa nini
    Haruki kwa kupotowa, bila kujuwa undani
    Pandisha nguo tarowa, maji yapanda mwilini
             Hayakupwi asilani

  2. Milango hujaijuwa, na dira za baharini
    Nyota hukuzielewa, mekupoteza mwinani
    Tafuta wanoelewa, wenye kuzama majini
    Ndipo hapo utajuwa, siri ya uvuvi nini
            Sirahisi asilani

  3. Uvuvi wako uzile, si samaki wa nyavuni
    Hufiki maji kule, marefu si ya fuoni
    Yakikupwa kachokole, chaza na pweza maweni
    Si changu na kolekole, si samaki wa fukweni
             Kiwataka baharini

Maher Fundi


Mvuvi kazama!!! (sikweli wajidanganya)


Date: 29 April, 2002

  1. Samaki uwavuao, wanishangaza mwenzangu
    Samakio si mwambao, wala hungoji kiwingu
    Kivulini ndio ngao, samaki wako wa changu

  2. Bahari uziendazo, ni za mbali kweli kweli
    Moyoni unayo nguzo, samaki wako ni ghali
    wewe huna matatizo, chumvi kwako si asali.

  3. Usemavyo ndio kweli, wendako huonekani
    Waepuka na ajali, kwani wangia kizani
    Ufanyayo ni halali, wabarizi barazani.

Hashil

 

  About Us | Poems | Privacy Policy | Contact Us | ©2004 Zanzinet
 

 

 

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet