.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Ndege Wangu Kanitoka

 

 

 

 

 

 

Related links

 

Ndege wangu Kanitoka...


Date: 22 Jul 2002

  1. Namiminika machozi, ndege wangu kanitoka
    Hadaa za mchuuzi, na posho za kila mwaka
    Za mtama na mbaazi, na nyingi nyingi nafaka
    Ndege wetu katutoka, hatunae mikononi.
  2. Toka kinda kamaizi, mithili panya na paka
    Akinitega kwa uzi, mitego mpaka fyuka
    Kila nilipobarizi, yeye alikwisha fika
    Ndege wetu katutoka, hatunae asilani.
  3. Ninapata kisuunzi, ya kale nikikumbuka
    Wakati tukila mbuzi, uhuru kushereheka
    Akapanga mapinduzi, kwa mapanga na mashoka
    Ndege wetu katutoka, hatunae abadani.
  4. Vidonda bado viwazi, ndipo alipotamka
    Ndege nipe nimuenzi, wewe ndiye wangu kaka
    Na ukifanya ajizi, tamuacha ataruka
    Ndege wetu katutoka, hatunae amanani.
  5. Tawaondoa walinzi, wale wangu nilokupa
    Niwaache majambazi, ulodhani wameng'oka
    Wairudishe mizizi, ubaki kuhangaika
    Ndege wetu katutoka, hatunae kataani.
  6. Kajifanya mfinyanzi, udongo akafundika
    Akayafunga mapenzi, pingu zisizofunguka
    Leo pataka hirizi, ndoa hii kudumuka
    Ndege wetu katutoka, hatunae tunduni.
  7. Akavinjari komanzi, ndege wangu kumnyaka
    Kawatia jinamizi, watetezi wa kichaka
    Akaukata mzizi, vyama vikaunganika
    Ndege wetu katutoka, hatunae milikini.
  8. Utamu wa maandazi, na makuku ya kupaka
    Karubuni walowezi, upofu kuwagubika
    Wasifanye yao kazi, ya ndege kumfunika
    Ndege wetu katutoka, hatunae hatunani
  9. Sasa hatuna pumzi, ndege wetu kasharuka
    Kufukuza hatuwezi, bahari kashavuuka
    Hata tukipiga kwenzi, harudi kashatoroka
    Ndege wetu katutoka, hatunae sikiani.

Maa salaam.

Kassim

Ndege wetu Katutoka...


Date: 22 Jul 2002

  1. Nimesikia yalokusibu, Hayajafika ya firauni
    Unyago isiwe sababu, Kuubeza utamaduni
    Kidegecho Kitaratibu, Kimeingia mwituni
    Kimezipata zabibu, harudi tena tunduni
  2. Ulijilabu kwa mikogo, Yuwako uhmo ndani
    Hilaki isio ndogo, Kumfungia bandani
    Kidegecho sio mfugo, Chataka ruka angani
    Kimezipata Zabaibu, Harudi n'go tunduni
  3. Japo kuwa ulikienzi, na kukipa kila raha
    Kilikosa usingizi, tunduni chaona karaha
    Kilijawa na simanzi, moyo ulijawa jaraha
    Kimepata zabibu, hakirudi tena tunduni
  4. Takupa langu jawabu, Ndege kiumbe adhimu
    hakitaki masharubu, Na ukali kama ndimu
    Hukawii kuharibu, Sifa na zake isimu
    Kimezipata zabibu, Harudi tena tunduni
  5. Ndege kazowea kuimba, Asubuhi na jioni
    Wewe umekifunga kamba, Kihoi tunduni
    Kakiokoa muumba, Na taabu za bandani
    Ndege sasa chajingamba, Harudi tena tunduni.

Nduguyo
Eddie Masoud.


 

 

 

  About Us | Poems | Privacy Policy | Contact Us | ©2004 Zanzinet
 

 

 

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet