.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Pakacha Pakachuka!

 

 

 

 

 

 

Related links

 

Pakacha pakachuka!


Date: 24/05/2002

  1. Pakacha waniweka, roho juu
    Pakacha kila mwaka, hata huu!
    Pakacha wanitaka, niwe zuu?
    Pakacha pakachuka, chini puu!
  2. Pakacha nadhikika, dhiki kuu!
    Pakacha ninanuka, na kupuu
    Pakacha wanicheka, sana tuu!
    Pakacha pakachuka, chini puu!
  3. Pakacha umeruka, kichuguu
    Pakacha hujavuka, lima kuu
    Pakacha 'tachauka, chau chau
    Pakacha pakachuka, chini puu!
  4. Pakacha sina shaka, si kifuu
    Pakacha asotaka, la mkuu
    Pakacha huvunjika, lake guu
    Pakacha pakachuka, chini puu!

Wassalaam.

Hassan,
Ottawa.

Pakacha pakachuka!


Date: 24/05/2002

  1. Tungo ni safi nzuri, ahsantuu
    Utunzi huna dosari, wewe juu
    Waenda njema safari, ya majuu
    Hassani wewe hodari, ni mkuu
  2. Beti zanukia wazi, karafuu
    Twafurahia ujuzi, ulio juu
    Furaha kubwa azizi, sikukuu
    Mkono wenye pongezi, shika huu

Shukran

Bakari A. Ali
Reading UK

Pakacha pakachuka!


Date: 24/05/2002

  1. Pakacha parachuka, wajikuta chini juu
    Pakacha lakucheka, mzegazeka nafuu
    Pakacha kusarifika, zambarau sio fuu
    Pakacha towa talaka, ndio siri ya kifuu
  2. Pakacha ni kichaka, cha mbuni vitu kuviacha wazi
    Pakacha mashaka, wengi wauza mbaazi
    Pakacha kushilanga muafaka, shabaha kupanda ngazi
    Pakacha kuliamini ni shaka, lageuka utelezi
  3. Pakacha nakunasihi, fujo zako kuziacha
    Pakacha huzimi wala huwashi, wajijua umechacha
    Pakacha kipimo chako ni pishi,wengine watoto pacha
    Pakacha ubani wako mafushi, mara nyengine mchicha
  4. Pakacha kujihashuwa uwache, mara hii utadunda
    Pakacha makarara kwako cheche, mnyama wako ni punda
    pakacha gari lako ni mkweche, wapakia vilovunda
    Pakacha miye si cheche, ni sungura kwenye sanda.

Wakatabahu

Hashil

Pakacha pakachuka!


Date: 25/05/2002

  1. Wallahi nafurahika, ushairi kuushika,
    Malumbano kuyateka, na nyoyo kuburudika,
    Ila Pakacha nateta, jawabu hatujalipata,
    Pakacha hili nlipi, la Canada au Pemba?
  2. Dr.nakukumbusha,pakacha la kwenu Pemba,
    Muhogo na wake pweza,jioni utajitweka,
    Masheli ya kupwaza,si haba utajitwika,
    Pakacha hili nlipi,mbona hwelitaja?
  3. Karafuu hichumia, na mpeta kuokotea,
    Leo mbona mwalinunia, pakacha hili la kujivunia,
    Wallahi najivunia, mipesa nejichumia,
    Dr.Hassan hebu nambia, kabla sijakufokea,
  4. Komputa hutaitia, ndani ya pakacha nakwambia,
    Ila ndio tweanzia, karafuu na kijio kutafutia,
    Hebu leo twambie, huko canada lipo hilo Pakacha
    Au nlile la aslia , Pemba na Unguja lanukia?

Wasalaam,

Ally Bin Aboubakar,
London.

 

  About Us | Poems | Privacy Policy | Contact Us | ©2004 Zanzinet
 

 

 

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet