|
|
Safari!
Date: 08 Oct 2002
Asalaam Alaykum
- Mbali yeanza safari, Pale tulipoamua
Wachache tulisafiri, kwa jahazi na mashua
Na manahodha mahiri, Tanga wakatutwekea
Iko siku tutafika, Baratu si mbali tena
- Tena si kwa mbali tena, Tanga tutapolitua
Mawimbi makubwa sana, Sasa yameshapungua
Ufukweni twapaona, Pale tutaposhukia
Iko siku tutafika, Kule tulokusudia
- Kule tulokusudia, Wenzangu si mbali tena
Mikaja kuikazia, Waume na wetu na wana
Nuru tushajionea, Na nyota zimejazana
Iko siku tutafika, Kwa nguvu za maulana
- Kwa nguvu za Maulana, Watoto Zinjibaria
Siku hiyo itafana, Sote tutafurahia
Kwa hatua za mwananai, Nyumbani tutaingia
Iko siku tutafika, Nyamaza twakaribia
- Nyamaza twakaribia, Ufukweni tutafika
Mama nyamaza kulia, Nguvuzo zahitajika
Tamati yanyemelea, Ikaribu kwa hakika
Iko siku tutafika, Kwa uwezo wa Jalia
Myonge wa Nyali New York
|