Chungwa: Bata: Jicho: Dunia: Kupenda: Kajificha: Pia (Ulimwengu wa Mashairi)
Date: 29 May 2002
Chungwa
Ladha ya chungwa si sawa, hata liwe susu moja
Utamu wa kila chungwa, walionja moja moja
Wala sijaota mbawa, nisemayo yanahoja.
Bata
Bata husemi ni kuku, jogoo kumwita paka
Mshuku si chuku, rafikiyo siyo kaka
Kiteweo chukuchuku, mke ataka talaka
Jicho
Jicho simaku adhimu, litumie kwa heshima
Usijitie wazimu, wakati unapolima
Bahati geuka sumu, unapopanda milima
Dunia
Nalizunguka dunia, kuitafuta bahati
Nikanunua gunia, yakawa kumbe machati
Katoka akaingia, mithili ya kalafati
Kupenda
Nakupenda hunipendi, nyimbo waloerevuka
Mapenzi siyo magadi, mdomoni kuyaweka
Wayaenzi kwa juhudi, siyo kutwa watapika
kajificha
Kajificha kwenye anga, ndege zinamtafuta
Wengine wamo kuanga, mafushi yao mafuta
Awangoja kwa mapanga, siku atayowakuta
Pia
Azunguka kama pia, dunia imemkumba
Wanatoka wakingia, waganga wenye vilemba
Lilobaki ni kulia, achombezwa na marimba.
Wakatabahu
Hashil