|
|
Unaniumiza Moyo!
Date: 1 Dec 2002
-
Umenipa mtihani, mgumu kuelezea
Sirahisi asilani, naogopa kutelea
Lakini nifanye nini, sina njia kurejea
Nakuomba niamini, sidhani najitetea
-
Sinacho chakukuficha, ikawa siri moyoni
Kila jambo nimeacha, umenitia mbioni
Nakesha usiku kucha, siyandoto niamini
Sina nilipokuwacha, nakuwaza mwafulani
-
Usisikize ya watu, wala rai sichukuwe
Watakuwambia kitu, ujiudhi uchukiwe
Laukweli sina mtu, nasitaki ila wewe
Iwe miaka mitatu, tasubiri unijuwe
-
Unaniumiza moyo, ukisema sikupendi
Mwenzio hali niliyo, sirudi wala siendi
Naingoja siku hiyo, naona siku hazendi
Naogopa watu choyo, kila kizidi kipindi
-
Ningeweza kufunguwa, ukapenya fuadini
Ukasoma nakujuwa, kilichondani moyoni
Wallahi ningepasuwa, kifuwa vipande chini
Ikawa yetu muruwa, kapata yako hanini
-
Pokea yangu ahadi, iko siku itafika
Dhamiri zetu tasudi, mikononi takuweka
Na uliko sibaidi, Mungu akishaandika
Tuvute zetu nyuradi, milango itafunguka
Maher
|