.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Vikuba Vilonukia

 

Related links

 

Vikuba Vilonukia!

Date: 20 Sep 2002

Viwapi vile vikuba, vilokuwa kinukia
Vilokitungwa kiriba, shingoni kining'inia
Kila kimwana kibeba, jioni ikiingia
Kikivaliwa kwa hubba, mume akafurahia
Usiku ukatimia

Vitalu vimeondoka, hakuna kilobakia
Wenyewe wametoroka, kwengine wamehamia
Waliko wajialika, kwa uturi kujitia
Moto nao waukoka, udi kujifukizia
Ndipo wanaponukia

Wamewaachia pumba, makapi ya vumbi lao
Wakifukiza ni vumba, harufu wanukiao
Wamo nao wajiwamba, wajihisi ndio wao
Kumbe mafusho wakomba, na udi hauko nao
Masikini roho zao

Maher

 

Vikuba vilonukia

Date: 23 Sep 2002

Sheikh Maher & wanaukumbi,

Vikuba uviulizavyo, viko kama kawaida
Haviuzwi ovyoovyo, wavipata kwenye shida
Ufahamu hivyo hivyo, wala sitaki ziada
Wamegubikwa na choyo, akili zao ni rada.

Vitalu bado tunavyo, majina yabadilika
Jela zaitwa mafunzo, ukingia waokoka
Wenyewe yao mawazo, wamebaki kumenyeka
Uturi kwao uwezo, paka mekoni acheka.

Waloacha hizo nyumba, ndani wakuta mitumba
Harufu kweli ya vumba, kama udongo wa shamba
Lilobaki ni kupamba, mapakacha na marimba
Wengine ngozi ya mamba, ukipita wakuimba.
 

Wakatabahu

Hashil

 

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet