.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Yamenishinda Wenzangu

 

Related links

 

Yamenishinda Wenzangu!

Date: 12 Aug 2002

  1. Haya yaliyonikuta, sihadithi ni ya kweli
    Nimarefu kuyaleta, kikubwa kitendawili
    Siyakuomba kumkuta, kwa yeyote ile hali
    Nauchungu nnajuta, kusema yote muhali
  2. Nilimgeuza ndege, tundu nikamjegeya
    Hati ya mambo msige, jina memuandikiya
    Kama yai kimuenge, kiogopa kuteleya
    Singoji nyayo ikanyage, kimuekea zuliya
  3. Yamenishinda wenzangu, mazito kifikiriya
    Hamupo pahala pangu, kwa dhati kuyahisiya
    Ukweli ajua Mungu, alivyo kinitendeya
    Kiniwacha peke yangu, nyumba kinielemeya

Maher

Yamenishinda Wenzangu!

Date: 13 Aug 2002

  1. Maher pole sana, kwa maafa yalokupata.
    Tena nasikitika sana, kwa hayo yalokukuta.
    Uchungu wake kifana, muasi huyo matata.
    Vizuri ulivyofanya, kumpatia talaka.
  2. Mwanamke memuenzi, kwa kila analotaka.
    Imanie jinamizi, moyo wake unawaka.
    Hana hata simanzi, hisia kuzikokota.
    Hurumae ibaidi, angalau kukupoza.
  3. Mke mwenye balaa, tamjua akipaa.
    Maneno yake alaa?, uso umekurupaa.
    Kumbe anaye balaa, mwenziwe wanayekaa.
    Maher sitaharuk haya, kula na unywe murua.
  4. Sali kiomba na dua, Mola atakushushia.
    Mabaya atakuvua, kheri atakuletea.
    Inshaalla utatulia, kwa rehma za Jalia.
    Ndoa utaifikia, na husda kukuondoshea.

CHAMA.

 

Zimenifika salaam

Date: 13 Aug 2002

  1. Salaam zimenifika, na wasia mepokeya
    Bi Chama,tawajibika, kwa kila ulonambiya
    Na yale memalizika, hakuna lilosaliya
    Tatu zote memtweka, talaka haikubakiya
    Kwaheri nimemwambiya
  2. Mfano wangu kizuka, nimo ndani nnatawa
    Mwenzangu mie mkeka, sala ikiadhiniwa
    Nafusi yafurahika, moyo wangu unapowa
    Maudhi huniondoka, kila niombapo duwa
    Namshukuru Moliwa
  3. Wakati utapofika, tatafuta ntaoa
    Sasa sinayo haraka, nadondoa kama chua
    Pupa,ntaghilibika, nisijuwe kuchaguwa
    Nami muhimu silika, natabiyae kujuwa
    Ndipo ntakapo powa

Maher

 

Yamenishinda Wenzangu!

Date: 14 Aug 2002

  1. Ni ajabu ilioje, vitimbi vya huyo mwana.
    Vyote apewa vereje, ikawa hatulizana.
    Auonapo uwembe, hujichinja kwa kuona.
    Yuradhi apawe pombe, sumuye asoiona.
  2. Mke uliyemtunza, vizuri ukamuweka.
    Leo aja kukutimba, kayda yake kidhaba.
    Hii yaonesha kwamba, imani yake ni haba.
    Na ukija kumkumba, pabaya atakuweka.
  3. ***************************

  4. Sura iliyo njema, husni tabia zake.
    Dini imemsimama, twayib ahli zake.
    Huyo ndie wa kusema, na kuarifiwa walid wake.
    Starehe yenye neema, mke na uzuri wake.
  5. Mtume hakukosea, aliyoyasema kuwa.
    Starehe ya dunia, mwema mwanamke oa.
    Mwenye dini na hisia, huruma kukuonea.
    Maher vumilia, huku ukizingatia.

CHAMA.

 

Yamenishinda Wenzangu!

Date: 15 Aug 2002

  1. Lau kama yu mkosa, asingeingia mtandaoni.
    Akaelezea visa, vya aliyekuwa shetani.
    Ambavyo vimemnasa, na kumkhasi moyoni.
    Ingekuwa hivi sasa, atanua viwanjani.
  2. Kutunga kwake shairi, si kuonesha fahari.
    Hadithi yake ya kweli, dukuduku lilo dhihiri.
    Ataraji zenu kauli, kujipoza muhadhiri.
    Siku zote neno zuri, huishinda sadaka yenye kiburi.
  3. ***************************

  4. Mwanamke huweza kuwa chanzo, cha mabaya na mazuri.
    Na kwake yeye ni chambo, kwa yule mwenye uzuri.
    endapo akenda kombo, mazuri hayatojiri.
    Labda afate mkondo, wa dini ulo mzuri.
  5. Mwanamke ana vituko, vikubwa anavyofiili.
    Na haya sio mashiko, bali ukweli kamili.
    Vya sheitani ni vituko, ni dhaifu na dhalili.
    Twayajua tokea huko, thibitisho la JALILI.

 

Chama.

 

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet