|
|
Chemsha Bongo!
Date: 12 August 2003
- Parakacha yuko chini, meno matatu yangoka
Aaga enda kazini, akutwa kwenye kichaka
Kakamatwa anazini, mke wa mwana Mashaka.
- Tabia yake uoza, ya wenziwe kuchunguza
Yake yamcheza, amungunya na kumeza
Mgonjwa kupeleleza, nyendo ni za pweza.
- Sefu amani amuri, mafya matatu kuweka
Pembua mwenye kiburi, chagua asomashaka
Tafuta pia ayari, alobaki kumuweka.
- Komamanga alipenda, shokishoki nazo pia
Matunda mengi apanda , mengine aagizia
Popote utaporanda, jina lake ni shezia.
- Mapenzi moto kifuu, yatia watu wazimu
Yakufanya ule fuu, uwe wino wa kalamu
Wengine kichefuchefuu, kulinda nyumba kwa zamu.
Hashil S. Hashil
Chemsha Bongo!
Date: 13 August 2003
- Mso hili ana lile, hakuna alotimia
Hayo yake maumbile, sisi sote twayajua
Usipige makelele, utaumiza kifua
Chuwa mezidi mchele, Vipi utazidondoa?
- Kiumbe huyo mzito, kuishi nae udhia
Huchemkwa na vukuto, ya watu kuyachungua
Kakaa kama mtoto, ni bora kumwachia
Atapewa mkong'oto, na mwalimu dunia
- Ngoma ikivuma sana, kupasuka ni dakika
Wangapi tulowaona, Vyeo wakijipachika?
Kijifanya maulana, na watu kiwatundika
Leo wametoka maana, wapita wafedheheka
Said Paul
Chemsha Bongo!
Date: 13 August 2003
- Hakuna kilichozidi, chumvi waweka mwenyewe
Wafanyao magaidi, mbinu zao ni za mwewe
Hutoa wao miadi, chuwa wewe uzitowe
Hayo kwao ni ya jadi, migombe isowenyewe.
- Kiumbe sio mzito, upekepeke mtamu
Mwishowe huwa majuto, sukari geuka sumu
Jiji huliwasha moto, wengine kuwapa pumu
Watu wazima watoto, zote hizo ni awamu.
- Avumae baharini, twaambiwa papa
Avumae majumbani, asomjua Mkapa
Avumae majiani, umma anaye wachapa
Avumae duniani, ni Bush kutapatapa.
Hashil S. Hashil
Chemsha Bongo!
Date: 13 August 2003
- Ya kweli uliyonena, na kasoro siioni
umenena yalo mboni, ajuae ameona
walikuwa juu sana, hawatuulizi sini
Leo hii hawanani, wamebakia kulana.
John Smith
Chemsha Bongo!
Date: 14 August 2003
- Leo nitakupa kisa, uwaelewe viumbe
Hii ni kweli kabisa, si uongo hata chembe
Wawili katika tisa, Ni wanyama waso pembe
Wamikia kutikisa, Niache leo niambe
- Nuhu Mtume wa Mungu, alikimbia gharika
Akayafuata mawingu, akafika pakufika
Akasema mlo wangu, njoo tuweni shirika
Kwani wetu ulimwengu, leo utabadilika
- Nanga walipoituwa, maskani walitaka
Kujisitiri mvuwa, Ikabidi kuezeka
Yale asiyoyajuwa, maombi akapeleka
Uwa aje kujengewa, Wapate kustirika
- Mafundi aliwapata, bila tabu na mashaka
Kilichompa utata, pale walipotamka
Binti yake kashata, mshahara walotaka
Nae bila ya kusita, Naam akaitika
- Wake mmoja binti, wote amewaahidi
Akayapiga magoti, kuongea na Wadudi
Najua kwako sitoti, Nimeshaweka ahadi
Kwangu wewe mlingoti, kurejea sina budi
- Mafundi walipongia, haki yao kuchukua
Chui na pundamilia, Kwa uwezo wa Jalia
Mabanati walikua, pasi kitu kupungua
Naye Mtume Nabia, Ndoa akawasomea
- Elewa sasa kwanini, watu wote sio sawa
Wengine ni hayawani, Chanzo chao kilikuwa
Wawenda ndani kwa ndani, kama mwasho wa chawa
Umshukuru Manani, kundi hilo kukutowa
- Taratibu ndio mwendo, mwenda pole hajikwai
Mambo sio kwa vishindo, pupa nayo haifai
Sharti uwe na miundo, Sio tu kujidai
Muwa ukizidi fundo, Mlaji huukinai.
Said Paul
Chemsha Bongo!
Date: 14 August 2003
- Kuna kiumbe Kijiwe, jina lak Barzanji
Kazi yake ni mayowe, kujifanya yeye jaji
Akilala ni kiwewe, akumbuka mauwaji.
- Mwengine Ame wa Pandu, mwendo wake ni wa tandu
Makali yake ya mndu, watu hawamuhusudu
Shepu yake ni ya ladu, ..........................
- Mengi tunayoambiwa, Amani kafilisika
Kaeni mukichunguwa, mtindi autandika
Mtuno wa kitumbuwa, wamuona watapika.
- Mkapa aenda kapa, daraja jina kujipa
Lipumba anamchapa, kukumbukwa kama papa
Kabakia tapatapa, wapinzani wameapa.
- Mwendo wa kobe haraka, kinyonga asingiziwa
Mke ataka talaka, ndowa asozitambuwa
Kazi kutupa mashaka, jambo hili kulijuwa.
Hashil S. Hashil
Chemsha Bongo!
Date: 15 August 2003
- Mvuvi nyavu karusha, zikazama baharini
Akangoja anakesha, mara aitwa majini
Afuta kanasa kasha, kufunguwa yumo jini
Kaanza kujichekesha, akamla kwa huzuni.
- Kisa cha pili porini, mnyama anaesema
Paa kutwa analani, viumbe wasohuruma
Mabunduki vichakani, nyuso zao kama chuma
Kwetu sisi visirani, watusaka wale nyama.
- Mtoto amezaliwa, kila dakika akua
Mdomo wake wa njiwa, wangara kuliko jua
Wazazi wakauguwa, waganga wakatambua
Muumba awazinduwa, kukumbuka wasojua.
- Kwenda mbio sikufika, kiumbe anza gutuka
Uendako utafika, wasia huo futika
Kinyonga anasifika, hakuna anomshika.
Dunia yatikisika, wamfata watapika.
- Miujiza ufukweni, simba kichwa cha samaki
Akapelekwa sokoni, kila mtu hamtaki
Akachomoza chetani, bei akatoa laki
Kamchukuwa mwituni, akageuka bunduki.
- Ladha haielezeki, kwa maneno kueleza
Itakufika hilaki, hata wasema wacheza =20
Kitu hicho hukiweki, chabaki harufu chenza
Ni mshindo wa fataki, wabaki kusikiliza.
- Vuta nkuvute, vyama viwili vikubwa
CCM iwe pute, CUF izidi kukuwa
Chakufanya tuwe sote, udhalimu kuungowa
Kijiwe kiwe cha wote, Muungano kuutuwa.
- Hakuna shida milele, tukipania kikweli
Tuyawache makelele, tupendane kweli kweli
Debe shinda jaza tele, mwenzio mpe ukweli
Tuyafukie ya kale, imani siyo ukali.
Hashil S. Hashil
|