|
|
Chombo Chaenda Mrama!
Date: 13 Feb 2003
- Naingia mitamboni, nazimwaga zangu beti
Nitoe yangu maoni, juu ya Zanzineti
Ya kuikaza demani, na kuziba kalafati
Chombo kiende sawia.
- Miaka ya tisiini, watu wakajizatiti
Kukitoa chelezoni, chombo hichi madhubuti
Wakakitia majini, kwa faida ya umati
Zanzibari wote pia.
- Azma yao makini, siyopitwa na wakati
Kwamba na sisi jamani, inatupasa kuketi
Kujadili kwa undani, ya Kojani na Kidoti
Kwa faida ya jamia.
- Yatokeayo nchini, pakawekwa mkakati
Kuyaleta ukumbini, ya ndani ya magazeti
Na yale ya mitaani, pasipo na vizingiti
Sote tupate sikia.
- Yakaletwa barazani, yakatipwa kitikiti
Ya akina Salmini, na Baucha Marikiti
Ya ndwele za matumboni, ya uhai na mauti
Ya huzuni na ya kufurahia.
- Wazawa wa Visiwani, tukapaaza sauti
Kuyasemeya kwa kani, tena bila ati ati
Yaliyojiri nyumbani, tukayakazia nati
Ya ratili na wakia.
- Tukifanya tathmini, kwenye yetu jamaati
Wako wanaoamini, wima tunapiga buti
Hatwendi tena usoni, twaliharibu busati
Mchele mezidi chuwa.
- Sababu yao yakini, migogoro haisiti
Habari za duniani, ndizo zilizo furuti
Zile za kwetu Mwambani, sasa zimekuwa seti
Malengo yanapotea.
- Wakikumbuka zamani, mwanzoni mwa hii neti
Michango ya kila fani, wala sio tashtiti
Ililetwa uwanjani, kwa mabunda na madoti
Mengi tukizingatia.
- Makala za ugenini, zenye uzuri wa hati
Mantiki hazilingani, macho yao hazivuti
Wajumbe wanatamani, maneno kama boriti
Mazima na yenye siha.
- Tulipo ndugu zanguni, yafaa kupiga goti
Tutafakari kwa shani, magamba na mitikati
Tusibakie kughani, yalaiti yalaiti
Chombo chaende mrama.
Kassim O. Ali
Limetumwa tena ukumbini na Maher
|