|
|
Fitina!
Date: 16 Oct 2003
- Fitina mtu khatari, siwezi kukhadithia
Mzushi hana nadhari, mjasusi wa kuzua
Anuka kama jodari, papa bovu la India
Fitina mvunja mji, umwonapo tahadhari.
- Fitina hana jeuri, usoni huchekelea
Hudai hana kiburi, laghai kunyenyekea
Hujifanya yu tayari, kitini kukwinukia
Fitina mvunja mji, umwonapo tahadhari.
- Fitina mtu ayari, heshi kukutembelea
Si mwema na si mzuri, hakai akatulia
Upole akuvinjari, apate kukuzulia
Fitina mvunja mji, umwonapo tahadhari.
- Fitina mfano ngiri, heshima hajatambua
Domo halitaghairi, kutoa yasio njia
Hata awe mshairi, fitina wote sawia
Fitina mvunja mji, umwonapo tahadhari.
- Fitina hana bahiri, maneno kupangilia
Fitina hana dosari, zaidi ya laki mia
Fitina katika pori, hukaa akangojea
Fitina mvunja mji, umwonapo tahadhari.
- Fitina si urafiki, ni utovu wa tabia
Halimukhusu fikiri, kwa nini kushikilia
Na kufanya dhamiri, kukaa kusimulia
Fitina mvunja mji, umwonapo tahadhari.
- Fitina khasa kafiri, karibu mwenye kuua
Huzikusanya khabari, kila pembe ya dunia
Uulizapo hakiri, adui wa watu pia
Fitina mvunja mji, umwonapo tahadhari.
- Fitina leo kariri, usome ukirudia
Ndoa ikisha shamiri, huwezi kuitangua
Ila atake Kahari, wakati ukiwadia
Fitina mvunja mji, umwonapo tahadhari.
- Fitina hii nadhiri, siku moja tatimia
kugundua ikijiri, kifungo nitachukua
Fitina hata tajiri, ras yake taitoa
Fitina mvunja mji, umwonapo tahadhari.
Eye Witness
|