|
|
HARUFU INONUKIA
Date: 02 May, 2003
Hili ni shairi nilotunga kuonesha jinsi mama mpenzi anavyompa wasia
mwanawe kutokana na majonzi na kumpa matumaini mema.
Mama uchungu, mama uchungu
yamala mwanangu, nyamala mwanangu
Tumbo la udere limauma mno eee
- Hamfunza mwana kulea,mtoto ameemewa
Hamfunza mwana tulia,mazuri yatawadia
Hamfunza mwana sikia,polepole hii njia
Harufu inowadia,vikuba vinonukia.
- Mwana tulia sikia,hao si wa kuridhia
Mwana hii ni dunia,mengi utajionea
Ni mama aniusia,haya nawahadithia
Harufu inowadia,vikuba vinonukia
- Ungama mwana kilua,maovu utajivua
Sisubu mwana wabua,wote waweza kulea
Kigota mwana kilia,kimya kimya yako njia
Harufu inowadia,vikuba vinonukia.
- Uyatunze yako mato,wabaya sijeyatoa
Ukate wako mkato,njia kuipalilia
Ugubike wako mto,kilala usiumia
Harufu inowadia,vikuba vinonukia.
- Mwana nilikuwa mwana,na mimi nikaelezwa
Wavyele walituwana,kwa kila tulilofunzwa
Kutapatapa kunena,ni zongo la kufukizwa
Harufu inowadia,vikuba vinonukia.
- Bwana kipeto mtua,na huku kichekelea
Tongoa uwe suria,anenalo kitendea
Mchago wako murua,imara wajiwekea
Harufu inowadia vikuba vinonukia.
- Ndwele ya nyumbani kwako,sitara waiwekea
Ubungo iwe ni mwiko,kukusanya hadhiria
Waramba kisogo chako,huku wakichekelea
Harufu inowadia vikuba vinonukia.
- Hewalla kubwa kauli,harufu yako nzuri
Isiwe tena kivuli,ukaharibu uzuri
Tohoa usikejeli,elimu ya ushazari
Harufu inowadia,vikuba vinonukia.
- Utote tote mluwa,vilua vyake murua
Kila pembe ina uwa,la waridi lachanua
Vikuba ukichukuwa,baridi vinonukia
Harufu inowadia vikuba vinonukia.
- Harufu tete ya pete,ngodani kichekelea
Kachiri ndani ya fete,kitoto kisherekea
Harufu doa lifute,nzuri inonukia
Harufu inowadia,vikuba vinonukia.
- Nyamala mwana kulia,mwanangu mekuridhia
Nyamala mwana tapoa,kheri ikikujilia
Nyamala mwana najua,vikubwa unaumia
Harufu inowadia,vikuba vinonukia.
SALMA KHAMIS
|