|
|
Ipokee Muadhamu
Date: 13 March, 2003
- Nnaishika kalamu, yaliyomo yafahamu
Haikuwa yangu hamu, kutaka kukudhulumu
Moyo wangu mah'mumu, bongo haliko timamu
Napenda yako kutimu, pokea hizi salamu
- Nayavuta kwa tadhimu, maneno yawe matamu
Upate 'ngiwa na hamu, uyasome ufahamu
Ondowa lako jukumu, kuwa hukunidhulumu
Moyo hauna matamu, umeamuwa kupumu
- Iko siku itatimu, furaha iwe timamu
Haitokuwa ya sumu, asali iliyo tamu
Hoja subira kutimu, taridhika muadhamu
Sasa naweka kalamu, najuwa tanifahamu
- Kwaheri ya kuonana, kiandikwa takuona
Na kwa sura kukutana, kwa marefu na mapana
Meno tutaoneshana, furaha zilofanana
Tumuombe Subhana, tupate kuja kutana
MIMINAE
|