.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Iweje Uwe Wa Tatu

 

Related links

IWEJE UWE WA TATU?

Date: 12 May, 2003

  • YA RABBY YA RAHMANY,NAANZA KWAKO MWENYEZI
    YA RABBY YA MUAWINY,KHERI ZAKO NIZIENZI
    YA RABBY YA MUFARIJANY,MUYASOME KWA MAKINI.
  1. Wewe sie mpangaji, ya watu kuwapangia
    Wewe sie mfunzaji, kidole kutunyoshea
    Najua yako juhudi, kwanini ukaumia
    Iweje uwe wa tatu, kutaka kutufitini?


  2. Pima ukizingatia, kweli yanaelekea?
    Vibaya kumkalia, mwenzio mwana sikia
    Wapita kila kijia, husuda kumtilia
    Iweje uwe wa tatu, kutaka kutufitini?


  3. Mola Jalla wa Azza, akujazi ewe mja
    baya kutufanyiza, kisimacho nawe chaja
    Wataka kwako kujaza, kwa mwenzio kukufuja
    Iweje uwe wa tatu,kutaka kutufitini?


  4. Ni bure unaumia, huna njema yako nia
    Wallahi nakuapia, na sala nakusalia
    Na mwenye kukusudia, baya kulisimamia
    Iweje uwe wa tatu, kutaka kutufitini?


  5. Isilamu wajigamba, mbona baya hukatazi
    Usimkae sambamba, mwenzio ana Mwenyezi
    Alotukuka Muumba, kaniongoza kwa ngazi
    Iweje uwe wa tatu, kutaka kutufitini?


  6. Tumeamua wenyetu, tena kwa hiari yetu
    Yanopita kati yetu, ni siri baina yetu
    Sijasikiapo katu, mke kuwa na watatu
    Iweje uwe wa tatu, kutaka kutufitini?


  7. Hebu soma historia, za waliotangulia
    Zama za ujahilia, zilipowatawalia
    Na ghafula kufikia, Amiri  kutarajiwa
    Iweje uwe wa tatu, kutaka kutufitini?



  8. Mimi nilivyofundishwa, chuoni na kwa malezi
    Isilamu muepusha, baya lisimtelezi
    Kheri zote kumvisha, kipata usimuudhi
    Iweje uwe wa tatu, kutaka kutufitini?


  9. Lakuuma la jamali, alilopata mwenzio
    Unatia na kejeli, ya nini dharau hio
    Unajifanya mkweli, Kama baya kwako sio
    Iweje uwe wa tatu, kutaka kutufitini?


  10. Unajifanya jabari, sio sifa yako hiyo
    Lakini nakusaili, mimi si mke mwenzio
    Nimefundishwa kauli, nzuri kuongea nao
    Iweje uwe wa tatu, kutaka kutufitini?


  11. Sitobishana kwa hili, nakueleza yaliyo
    Mikono hii miwili, uu kielekea kwayo
    Namuomba ya KAHARI, akuondolee  CHOYO
    Iweje uwe wa tatu, kutaka kutufitini.


  12. Sisi tunaye MUUMBA, Inshaallah tatuongoza
    Yako uliyoyakumba, gizani ulikofunzwa
    Shuhuda wa hii nyumba, shahidi wataongoza
    Iweje uwe wa tatu, kutaka kutufitini?

SALMA KHAMIS.

 

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet