|
|
KIMBUNGA
Date: 25 August, 2003
-
Kimbunga mji wa Siyu, kilichowahi kufika
Si kwa yule wala huyu, ilikuwa patashika
Kimeing'oa mibuyu, minazi kunusurika!
- Yalizuka majabali, yakabirukabiruka
Zikadidimia meli, ngalawa zikaokoka!
Kimbunga hicho kikali, mavumbi hayakuruka!
- Nyumba kubwa za ghorofa, siku hiyo ziliruka
Zikenenda kwa masafa, kufikia kwa kufika
Vibanda vyao malofa, vyote vimenusurika!
- Chura kakausha mto, maji yakamalizika
Pwani kulikuwa moto, mawimbi yalivyowaka
Usufi nusu kipeto, rikwama limevunjika!
KIITIKIO:
Usufi nusu kipeto, rikwama limevunjika!
Chura kakausha mto, maji yakamalizika!
Kutoka kwa Bwana Haji Gora Haj
Limeletwa na Hassan O. Ali
|