|
|
Linanukiya Miyaka
Date: 18 March, 2003
- Najuwa unaniona, ni mbele machoni mwako
Si mbali,karibu sana,ni kope na mboni zako
Nami sina la kunena, nakusikiya uliko
Ukitaja langu jina, naitika huko huko
- Kikohowa nashituka, haraka hukuitika
Roho ikashugulika, kujuwa nini wataka
Wasi wasi hunishika, moyo hunipaparika
Mbio nikakurupuka, vyumbani ingiya toka
- Fahamu zangu huruka, zikirudi nikacheka
Kuwa nnahangaika, nawe hupo kwa hakika
Chako kimenifunika, kivuli menitandika
Sina nnachokumbuka, ila wewe sina shaka
- Huwa nawe kisinziya, ubavuni chini yako
Mikono hukuwekeya, kipakata kichwa chako
Ukawa wanilekeya, nami haeleka kwako
Huku nikikubembeya, ulale kwa raha zako
- Ni ndoto iliyo refu, iso mwisho na mpaka
Yenye masafa marefu, tusoweza kuyafika
Si jambo kuwa halafu, litaweza kamilika
Ni huba lenye harufu, linonukiya miyaka
- Usikae ukaliya, wala ukasikitika
Nafahamu waumiya, roho yako inalika
Ilo bora Vumiliya, yetu siku itafika
Wakati ukiwadiya, kwa shangwe tafurahika
- Yako yananiunguza, machozi yakikutoka
Huyahisi kichuruza, tone tone kidondoka
Ya moto nikiyapoza, kifuani kibabuka
Usione menyamaza, nakwisha namalizika
Maher
|