|
|
Naitamani Sauti!
Date: 09 Feb 2003
- Ndege uliye angani, Kiringia hewani
Sauti yenye kughani, inaponitoa ndani
Nikaapo dirishani, Isishe nnatamani.
- Urukapo kwa madaha, asubuhi na jioni
Sauti yenye furaha, hupita masikioni
Nami huona raha, isimalize natamani.
- Napenda yako sauti, aliyokupa Manani
Nami nikaja kititi, kubaini yako shani
Mola kakupa sauti, nzuri naitamani.
- Ndege wanibembeleza, asubuhi na jioni
Nami sina cha kuwaza, Nikuonapo waghani
Sauti huniliwaza, Kunitoa majonzini.
- Ndege nakuomba pita, jioni imewasili
Mazuri yakufuata, Sauti meisabili
Mikono imefungata, mtama wakusubiri.
- Moyo meingiwa wahka, njoo mbawa zako mbili
Hakuna ataekupa, Mazuri nakusaili
Kubwa ndani kukufunga, nje uione mbali
Usiwe na mhimili.
- Ushindwe pa kupapasa, mti uuone mbali
Urudi ninakuasa, Tizama yaliyo mbali
M-baya akikunasa, atakukata kilimi
Usiweze na kughani.
- Ndege meumbiwa anga, Utandie na ughani
Usiwe ndege kubanga, alojitoa thamani
Akashindwa ya kupanga, akaleta tafrani.
- Ndege uliye adhimu, Sauti yako ni tamu
Asubuhi wasalimu, Jioni nayo timamu
Umeumbwa na KARIMU, Sifa usiituhumu
Sauti yako ni tamu, Njoo unikirimu.
- Imba unipe raha, na uruke kwa furaha
Macho yenye madaha, yakuangaze kwa raha
Moyo mejawa furaha, Natamani zako raha.
- Njoo unipe furaha, Kwa sauti ya madaha
niokoe na fadhaa, Dirisha nilipokaa
Kimya chako si ridhaa, Na si yako khulka.
- Au kama mekosea, Sina budi kukwambia
Samahani ipokea, Moyo wako ufumbua
Ndege unayeenziwa, Au Hajj umekuwa?
Umenipa mazowea, Nashindwa kujitambua.
- Sauti yako ni neema, ni dua kwa masikini
Asubuhi ukinena, Mchana nauthamini
Jioni ukiitema, Kwa nyimbo zenye thamani.
- Sili nisipokuona, Ukirukia angani
Moyo unasonona, Sauti naitamani
Ndege ninakutamani, Sinitie hamkani
Nipo hapa dirishani, macho kiangaza hewani.
Chama
|