|
|
Nakutafa uliko
26 Jan 2003
- Ndege wangu ndege wangu, nakutafuta uliko
Nakuapia kwa mungu, moyo wangu uko kwako
Sinipe kizungu zungu, kunitangisha mwenzako
Nakuhitajia kwangu, Nizipate raha zako
- Memaliza ulimwengu, sijapata fani yako
Nimeipanda mikungu, kitizama kama uko
Macho mefanya kiwingu, hayaoni kwengineko
Urudi kipenzi changu, unienzi niwe wako
- Sisikize walimwengu, kutupa mahali pako
Siharibu pendo langu, urudi hapa niliko
Nikuenzi mboni zangu, ukijue cheo chako
Nawangiwe na machungu, moyo mesabili kwako
- Mewapiku kwa mizungu, turufu zote n zako
Niradhi nitiwe pingu, sirudi nyuma mwenzako
Rejea nyumbani kwangu, nichezee mbawa zako
Wewe ndie ndege wangu, simtafuti mwenzako
Miminae
|