|
|
NAKUTAMANI MWANDANI
Date: 18 March, 2003
- Hadhira ninaijuza, kwa yote niliyofunzwa.
Mapenzi niloyakuza, mwandani kumliwaza.
Ni pekee nayatunza, yako nimeyatukuza.
- Yangu ya ndani fuadi, naahidi takuenzi.
Mapenzi yaloshtadi, si kwa sababu simanzi.
Lisanio meshadidi, nyamae nzuri azizi.
- Mwandani ulo wa ndani, wangu ninakutamani.
Baidi yako hanini, nakupenda niamini.
si yeyote insani, aliyekuzidi mwandani.
- Mapenzi yako mwandani, yanaishinda asali.
Mapenzi yenye imani, thabit tena ya kweli.
Mpenzi nakutamani, kwa yeyote ile hali.
- Nashindwa kujitambua, Nashindwa kuvumilia.
Natafuta kila njia, Ridhaa kuifikia.
Tafrani nimekuwa*azizi nakuhitajia.
- Natamani ya mwandani, Naumia kwa mwandani.
Ungefungua moyoni, ukaona tathmini.
Kwa ninavyokuthamini, Nakutamani mwandani.
- Mwandani usinikhini, nakuomba niamini.
Umuamini Manani, Nakulia na yamini.
Ni kubwa yako thamani, hakika nakuthamini.
Pokea hii zawadi.
Wengi hawaifaidi.
Nyoyo zao hufisidi.
Na chuki zao huzidi.
Waitafuta kwa dhati, Na kwa miguu ya futi.
lakini hawaipati.
SALMA.
NAKUTAMANI MWANDANI(JIBU)Date: 18 March, 2003
- Mwenzetu ulivyorowa, chapachapa hujiwezi
Mapenzi yakukongowa, umekonda kama uzi
Dawa yakukuokowa, kumsahau mpenzi.
- Mapenzi yakitoweka, kuyarejesha udhia
Hugeuki malaika, kazi kiguu na njia
Pakucheka watapika, ndani kwa ndani walia.
- Huwi wewe ni wa kwanza, wengi wameangamia
Gonjwa mapenzi lameza, lakuchoma kishazia
Lilobaki kujikaza, mwishowe lakuwachia.
Hashil
|