.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Ndege Unayetafutwa

 

Related links

Ndege Unayetafutwa

Date: 28 Jan, 2003

  1. Ewe ulobahatika, ndege uliye hewani
    Unopita ukiruka, na kuranda mitaani
    Mwenzio ahangaika, aparamia mitini
    Fanya urudi haraka, zikuone zake mboni

  2. Fani yako memponza, memuathiri moyoni
    Dunia kaimaliza, kwa wengine hulingani
    Na sasa wamuumiza,'akutaka,hakuoni
    Jaribu utavyoweza, ungie mwake tunduni

  3. Fuadi kitanda chako, yeye kakutandikiya
    Kifua ndicho tandiko, chake kakuzawadiya
    Mwengine kwake hayuko, wewe mekusabiliya
    Wafanya nini uliko?, hwendi ukamridhiya

  4. Lau moja mevunjika, ya pili mbawa rukiya
    Ano'itwa huitika, labeka huitikiya
    Huwa hafanyi dhihaka, huenenda kisikiya
    Nawe jihimu shituka, ushike wangu wasiya

  5. Bahati mekugongeya, iko pako mlangoni
    Sioni cha kungojeya, na kuchelewa njiani
    Naona waichezeya, shilingi yako chooni
    Ikangia mepoteya, ndio basi huioni

Maher Fundi

 

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet