|
|
Ninani Dhaifu Miye!
Date: 26 Feb 2003
- Bismillahi Wadudi, Allahu Rabbi Khaliki
Kwa haki nakuhimidi, Allahu hugawanyiki
Umpweke u Wahidi, huna haja huna dhiki
Ewe Mola Mutaali, pokea ungamo hili.
- Ninani dhaifu miye, sijiwezi sijishiki
Ninani hakiri miye, sitoi na similiki
Ninani fakiri miye, sina kile sina hiki
Ewe Mola Mutaali, sikiza ungamo hili.
- Sikiza ungamo hili, kama ni yangu laiki
Hizingatia mawili, ya mimi nawe Khaliki
Nakiri huna wa pili, U Pweke Mola Maliki
Ewe Mola wa Ukwasi, pokea ungamo hili.
- Naungama takiraba, haja kwangu imesaki
Rabbi Bwana wa Qaaba, mja nimejaa dhiki
Bila Wewe sina heba, maadumu makhuluki
Ewe Jallahu Jalali, sikiza ungamo hili.
- Nimedhoofu nafusi, inanichoma mikuki
Vipi mja nakuasi, kwendekeza uzandiki
Kama si Kwako Quddusi, kwa nani kuso mfaki?
Ewe Rabbana Rahimu, pokea ungamo hili.
- Najidhalilisha Kwako, Ya Rabbi Mstahiki
Ninanyenyekea Kwako, Ya Rabbi Dhati ya Haki
Kila kiumbe ni Chako, Ya rabbi unomiliki
Ewe Qadiru Qahari, sikiza ungamo hili.
- Mja kamwe hafanani, hata hafananishiki
Na dhati yako Manani, hata halinganishiki
Hutaniacha njiani, si kufu yako Razzaki
Ewe Mola wa Ukwasi, pokea ungamo hili.
Ahmed Rashid
|