.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Twawalalia

 

Related links

TWAWALALIA

Date: 1 April, 2003

NALIA JAMA NALIA

  1. Nalia jama nalia, msambe ninakufuru.
    Da'salaam metujia, misiba kwa msururu.
    Giza sasa tajitia. metoweka yao nuru.
    Wastiri Ya Kaharu, Dua yetu kwa pamoja.
  2.  

     
  3. Wastiri Ya Kaharu, Dua yetu kwa pamoja.
    Hawana tena uhuru, kukuomba zao haja.
    Hivyo sisi twawazuru, maana bado tu waja.
    Wastiri Ya Kaharu, Dua yetu kwa pamoja.
  4.  

     
  5. Wa kwanza kumsikia, ni Sheikh Bin Nassoro.
    Wengi tukamlilia, akatutia kihoro.
    Alimu wa asilia, katuachia kasoro.
    Wastiri Ya Kaharu, Dua yetu kwa pamoja.
  6.   

  7. Na wapili kututoka, ni Ustaadh Mtengwa.
    Mwalimu wa kusifika, kauli isiyopingwa.
    Nyadhifa nyingi kashika, mwanaharakati bingwa.
    Wastiri Ya Kaharu, Dua yetu kwa pamoja.
  8.  

     
  9. Mzee wetu Mwilima, ameongeza idadi.
    Atakumbukwa daima, kwa uongozi stadi.
    Wala hakurudi nyuma, kuondosha ufisadi.
    Wastiri Ya Kaharu, Dua yetu kwa pamoja.
  10.     

  11. Wote hawa mahodari, kujenga Uisilamu.
    Waliokuwa tayari, kuelimisha kaumu.
    Na kupambana na shari, kutimiza majukumu.
    Wastiri Ya Kaharu, Dua yetu kwa pamoja.
  12.   

  13. Rabi Mola Bwana wetu, twakuomba Ya Manani.
    Siwape adhabu katu, uwapeleke peponi.
    Wawe pamoja na watu, walofuzu kiimani.
    Wastiri Ya Kaharu, Dua yetu kwa pamoja.
  14.   

  15. Na pia uzinusuru, jamii za marehemu.
    Wakubali washukuru, majonzi kwao sidumu.
    Yasije yakawadhuru, nafsi kuzidhulumu.
    Wastiri Ya Kaharu, Dua yetu kwa pamoja.
  16.   

  17. Na sisi tuliobaki, tupe ari na subira.
    Kupambana na mikiki, kwa hekima na busara.
    Tuwashinde mamluki, na kuwatia hasara.
    Wastiri Ya Kaharu, Dua yetu kwa pamoja.
  18.   

  19. Alilopanga Jalia, twatakiwa tushukuru.
    Roho ziwe maridhia, kwa kila atoamuru.
    Hata kama ni tanzia, tusione atudhuru.
    Wastiri Ya Kaharu, Dua yetu kwa pamoja.   

  20. Misiba siyo kioja, toka kale hadi sasa.
    Lililo bora kwa mja, kujiandaa kabisa.
    Ili mauti yakija, awe nazo nyingi hisa.
    Wastiri Ya Kaharu, Dua yetu kwa pamoja.
  21.     

  22. Ilisemwa vitabuni, kama mauti lazima.
    Injili na Furkani, Taurati zimesema.
    Na Zaburi kubaini, kwa kauli ya Hashima.
    Wastiri Ya Kaharu, Dua yetu kwa pamoja.
  23.   

  24. Tamati nimefikia, naziomba zenu Dua.
    Mauti yakinijia, Mola kuja nichukua.
    Pazuri nije fikia, roho yangu ijetua.
    Wastiri Ya Kaharu, Dua yetu kwa pamoja.
  25.  

Kutoka kwa Assad Abdallah Kipanga
  Imeletwa na Saleh Barkey

 
Top
  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet