.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Ujana

 

Related links

UJANA

Date: 06 May, 2003

  1. Ujana kitu kitamu, tena ni azizi sana
    Maungoni mwangu humu, nilikuwa nao jana
    Kwa wingi katika damu, tahamaki leo sina!
    Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.


  2. Kichwa kimejaa mvi, kinywani meno hamna
    Nikenda kama mlevi, miguu nguvu haina
    Kumbe ujana ni hivi, ukenda hauji tena!
    Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.


  3. Jua langu limekuchwa, na nyota nilizoona
    Ukinitizama kichwa, nywele nyeusi hakina
    Kama zilizofikichwa,zikang'olewa mashina
    Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.


  4. Natatizika kauli, midomo najitafuna
    Nimekusanya adili, walakini hali sina
    Dunia kitu bahili, hiki una kile huna!
    Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.


  5. Nilikuwa ni waridi, furaha ya wasichana
    Neno hawakunirudi, wakati wa kukutana
    Sasa nanuka baridi, wanionapo waguna
    Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.


  6. Walio wakinibusu, walikuwa wengi sana
    Wanawake wenye busu, uzuri na usichana
    Sasa sina hata nusu, ya wanitajao jina
    Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.


  7. Wazuri wenye uturi, na mikono yenye hina
    Kila mtu mashuhuri, alipenda kuniona
    Nilifaa kwa shauri, na sasa sauti sina
    Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.


  8. Dunia bibi arusi, kwa watu kila namna
    Inapendeza nafsi, wakati wa kuiona
    Na leo sina nafasi, kwa uzee kunibana
    Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.


  9. Kilichokuwa gizani, niliweza kukionap
    Nikakijua thamani, sura yake hata jina
    Sasa sijui ni nini, hata ikiwa mchana
    Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.


  10. Kilichotaka fikira, niliweza kukinena
    Kwa mfano na kwa sura, mpaka kikafanana
    Leo tazama hasara, nguvu hiyo sina tena
    Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.


  11. Kilichotaka mapimo, sikifahamu mapana
    Marefu yake na kimo, siifahamu bayana
    Nusu nimo nusu simo, duniani najionap
    Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.


  12. Hadumu nasikitika, rafiki yangu ujana
    Machozi yamiminika, na la kutenda hapana
    Ni wakati umefika, uzee dawa hauna
    Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.


  13. Hauna dawa uzee, mabega yamepetana
    Anionaye ni"wee!, ondoka hapa laana"
    Wanaposema na miye, niliyekuwa na jina!
    Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.


  14. Wakatabahu shairi, uchungu wanitafuna
    Walakini nafikiri, twafuata Subuhana
    Katika ile amri, ya"kuwa"na "kutengana"
    Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

Shairi la Shaaban Robert
Limeletwa na Maher

 

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet