|
|
Unaniumiza moyo
Date: 1 March, 2003
- Umenipa mtihani, mgumu kuelezea
Sirahisi asilani, naogopa kutelea
Lakini nifanye nini, sina njia kurejea
Nakuomba niamini, sidhani najitetea
- Sinacho chakukuficha, ikawa siri moyoni
Kila jambo nimeacha, umenitia mbioni
Nakesha usiku kucha, siyandoto niamini
Sina nilipokuwacha, nakuwaza mwafulani
- Usisikize ya watu,wala rai sichukuwe
Watakuwambia kitu,ujiudhi uchukiwe
Laukweli sina mtu,nasitaki ila wewe
Iwe miaka mitatu,tasubiri unijuwe
- Unaniumiza moyo,ukisema sikupendi
Mwenzio hali niliyo,sirudi wala siendi
Naingoja siku hiyo,naona siku hazendi
Naogopa watu choyo,kila kizidi kipindi
- Ningeweza kufunguwa,ukapenya fuadini
Ukasoma nakujuwa,kilichondani moyoni
Wallahi ningepasuwa,kifuwa vipande chini
Ikawa yetu muruwa,kapata yako hanini
- Pokea yangu ahadi,iko siku itafika
Dhamiri zetu tasudi,mikononi takuweka
Na uliko sibaidi,Mungu akishaandika
Tuvute zetu nyuradi,milango itafunguka
SALMA KHAMIS (CHAMA).
|