.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Binaadamu Bora Mimi

 

 

 

 

 

 

Related links

Binaadamu Bora Mimi

Date:  16 May 2004

Wana-Zanzinet na Wapenzi wa Mashairi,

Assalaam alaykum.

  1. Boramimi bin'adamu, napenda jiweka kati
    Na kutukuza isimu, yangu bila ati ati
    Na kujiona muhimu, wengine wote makuti
       Udhaifu mtikati, boramimi bin'adamu
  2. Na ile yangu kaumu, taisomea kunuti
    Ibariki na kudumu, kuishinda Imarati
    Ndiyo jamii adhimu, taibeba kitikiti
       Udhaifu mtikati, boramimi bin'adamu
  3. Kila ninapostakimu, ninachunguza kwa chati
    Ni nani mwenye kukimu, wa mali na nyingi noti
    Nani mwingi wa elimu, nani mbovu wa goti
       Udhaifu mtikati, boramimi bin'adamu
  4. Nitatafuta kwa hamu, wasifu na zao nyeti
    Mali mwenye kuhizimu, tamheshimu kwa dhati
    Ama akinidhulumu, tamchomea baruti
       Udhaifu mtikati, boramimi bin'adamu
  5. Mwenye nguvu taheshimu, lakini tajizatiti
    Na hata kama sitimu, urefu wa tatu futi
    Hilo halijawa gumu, taongezea majiti
       Udhaifu mtikati, boramimi bin'adamu
  6. Kijaaliwa fahamu, nikasoma darasati
    Ninajiona mwalimu, mjuzi wa kila hati
    Wengine wote mabomu, tawakanyaga kwa buti
       Udhaifu mtikati, boramimi bin'adamu
  7. Na yule alonisumu, katu sitomsaliti
    Tamuenzi mahmumu, yeye wangu mwanasiti
    Yeye ndie muadhamu, sitofanya tashtiti
       Udhaifu mtikati, boramimi bin'adamu
  8. Tamuenzi nimchumu, hata kama simpati
    Sifaze tatarakimu, pasi kukosa wakati
    Tamwandalia karamu, nimpe na yangu voti
       Udhaifu mtikati, boramimi bin'adamu
  9. Hata wengi kilaumu, swahibuyo afiriti
    Ndipo nitapoazimu, kumjaza kalafati
    Katu hamnikhasimu, na huyu wangu banati
       Udhaifu mtikati, boramimi bin'adamu
  10. Lakini nisomhamu, katika huu umati
    Hata akijaza fomu, awe wangu hazarati
    Tatamani mpa sumu, yamfikie mauti
       Udhaifu mtikati, boramimi bin'adamu
  11. Wewe mwana wa Adamu, wabweka wala hujuti
    Waabudu ya nujumu, na ubinafsi huwati
    Humchi Mola Karimu, hadi uwe makhtuti
       Udhaifu mtikati, boramimi bin'adamu
  12. Mezoea kuhukumu, na kuzigawa jamati
    Uyaonayo matamu, yatafikia tamati
    Ndipo itapolazimu, safari bila tiketi
       Udhaifu mtikati, boramimi bin'adamu
  13. Niliyotongoa humu, si sera si mikakati
    Si hoja wangu wa damu, kuafiki zangu beti
    Ninaibwaga kalamu, sasa nakwenda kuketi
       Udhaifu mtikati, boramimi bin'adamu

Maa salaam.

Kassim

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet