|
|
Bure Sinikadhibishe
Date: 19 August, 2004
- Bure sinikadhibishe, kunitia uongoni
Wala sijibabaishe, mimi nimekuoneni
Katu sjikurupushe, mekukuta mikononi
- Nyendo zako mezijua, nalibaini zamani
Juhudi nikachukua, kuitafuta yakini
Sasa nimekutambua, kama wewe ni Khaini
- Haya zimekuondoka, ukasahau hisani
Huruma zikakutoka, wema usiuthamini
Leo unababaika, unajuta kitu gani
- Wallahi nakuapia, umejitowa thamani
Kwa mbaya zako tabia, na wingi uhayawani
Uzuri wako zulia, makazi yako ni chini
Kiitikio:
- Ni bure hiyana yako, ubaya kunifanyia
Nimempata mwenzako, mwenye sifa na tabia
Shairi la Ahmed Khamis Al Barwani
Limeletwa na Maher Fundi
|