|
|
FISI AKILA MUWELE
Date: 07 August, 2004
- Tunyamazile hatwambi, wala sidhani tulele
Twamuatia mlumbi, mwenye kusema milele
Tumevuwata mafumbi, na maozi yatulile
Fisi akila muwele, mzima funga mlango
- Sisi hatuvundi kambi, shahidi ashuhudile
Wala hatuna vitimbi, mwengine kumtenzile
Ingawa tunavyo tumbi, kufanya tuliketeke
Fisi akila muwele, mzima funga mlango
- Twazitunga zetu ngambi, tangu zamani za kale
Na sharuti za ukumbi, twaziswarifu vi' vile
Kuchelea kalima mbi, kuzitupa mbelembele
Fisi akila muwele, mzima funga mlango
- Mola hatizami sura, na nasabuyo swafile
Atizamalo Qaraha, ni nyoyo ziso na tule
Usiandame ghurura, fikiri nyuma na mbele
Fisi akila muwele, mzima funga mlango
- Wangapi walo wabora, na vyeo vya kulekele
Kwa kuandama ujura, mangi yamewapotele
Hawakufidi tijara, ilobaki ni kelele
Fisi akila muwele, mzima funga mlango
Maher Fundi(Unique)
|