|
|
KINU KIMEVUNJIKA
Date: 13 November, 2004
- Ndugu zangu sikieni, ninatafuta shauri,
Wataalamu changieni, mniepushie shari,
Wenye Elimu ya dini, na hata madakitari,
Kinu kimevunja mchi, kutwanga hakutwangiki!!
- Nina nafaka ghalani, za mahindi na mpunga,
Na nyingi ziko shambani, katika vyangu viunga,
Ninahitaji maoni, mnaojua kutunga,
Kinu kimevunja mchi, kutwanga hakutwangiki!!
- Ni mgumu si laini, hivi leo umepinda,
Sijui nifanye nini, mchi wangu naupenda,
Nitumie mbinu gani, kwa upya nikauunda,
Kinu kimevunja mchi, kutwanga hakutwangiki!!
- Tatizo hili ni geni, halikuanza zamani,
Na kinu hiki si duni, ni changu hapa nyumbani,
Natwangia kwa makini, asubuhi na jioni,
Kinu kimevunja mchi, kutwanga hakutwangiki!!
- Kinu hiki kina nini, au tatizo ni mchi,
Ni njama yake jirani, nikamkatie pochi,
Kutwanga ninatamani, hilo mimi siwafichi,
Kinu kimevunja mchi, kutwanga hakutwangiki!!
- Maji kidogo kinuni, kutwanga kuwe rahisi,
Tatizo lake ni nini, nimepatwa wasiwasi,
Au hili jini gani, au ni yule chunusi,
Kinu kimevunja mchi, kutwanga hakutwangiki!!
- Shime shime wa jamani, mnijibu kwa makini,
Mazao yalo ghalani, kutwanga ninatamani,
Mniondolee soni, nirudishie imani,
Kinu kimevunja mchi, kutwanga hakutwangiki!!
Shairi la Mwanakijiji
Limeletwa na Walii Genderi.
|