.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Kuandika

 

 

 

 

 

 

Related links

Kuandika

Date:  27 April 2004

  1. Uandishi una meno, wataka nyingi hikima
    Usanifu wa mikono, umahiri uso kima
    Ustadi wa maneno, na msamiati mwema
    Uandishi ni sanaa!
  2. Uandishi ni hazina, haipatikani bure
    Hii ni bahari pana, si bakuli la kaure
    Wavuao wakavuna, sio wavuvi uchwere
    Ni wajuzi wa sifa!
  3. Kuandika ukasibu, uliyonayo moyoni
    Wakakiri masahibu, na vijana viamboni
    Ni kama vile zabibu, zilizoiva mtini
    Zimetunzwa zikapea!
  4. Andikeni kwa muala, vifungu hadi vituo
    Yapangeni masuala, kwa makara na mapeo
    Sio kama majalala, yakaja kwa mkupuo
    Bila ya kuongozana!
  5. Hata hivyo nawaasa, uandishi una hulka
    Kitokea kudodosa, kalamu ikakutoka
    Vyema kukiri makosa, kuliko kuaibika
    Kwa kutaka kubishana!
  6. Muandishi muungwana, hafanikiwi kwa ngumi
    Huandika yenye maana, pasi nyanyua ulimi
    Sadifu kuwa mwanana, mahakimu ni wasomi
    Wasomi na jamii pia!
  7. Siwachoshe bobo yangu, vidole ninavitua
    Namuomba mola wangu, anipe kubwa hatua
    Nijue ya Ulimwengu, na mbinu za kutongoa
    Mbinu na kauli thabit!
  8. Rabi nijaalie mimi, na kila mwenye kusoma
    Tuondolee vichomi, tuandike yalo mema
    Rabi zidni ilmi, warzukna fahama
    Aaamin!

 

Kassim O. Ali

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet