|
|
KIMEPOTEA MACHONI
Date: 26 September, 2004
- Lau kuwa ni adimu, kitu nikakitafuta
Mapema nikafahamu, kilipo nikakifata
Ikatoka yangu hamu, nnachotaka kupata
Au nikangoja zamu, ikafika sijajuta
- Kimenitoka machoni, mbali na upeo wangu
Naangaza sikioni, hakipo,simbele yangu
Kimenifunga moyoni, kwa dhana ati ni changu
Sinacho nifanye nini, nawauliza wenzangu
- Kimeibiwa mchana, kweupe nje pepepe
Hakuna kino fanana, mfano wake niwape
Naogopa raha sina, alo kiba asitupe
Kikaokotwa na wana, nikabakia mweupe
Maher Fundi(Unique)
KIMEPOTEA MACHONI
Date: 27 September, 2004
- Utulize moyo wako, kilicho chako ni chako
Sijitie sumbuiko, kuutesa moyo wako
Madhali ni haki yako, kilipo tarudi kwako
Halijawa sokomoko, lihifadhi chozi lako.
- Konde upige mtima, kisicho chake si chake
Ngangari wima simama, sijali papara zake
Haki hutwawa nzima, simwombe haki si yake
Halijawa sokomoko, lihifadhi chozi lako.
- Kingakutoka mbonini, visivyo ndivyo vilivyo
Ni shari ungaidhani, sivyo ni kheri ilivyo
Asau ya Rahmani, subiri itakiwavyo
Halijawa sokomoko, lihifadhi chozi lako.
Ahmed Rashid
KIMEPOTEA MACHONI
Date: 28 September, 2004
- Unakitafuta nini, na kitu kimikononi
Humuhitaji jirani, unacho na kimo ndani
Kishafahamu yakini, siingiwe na huzuni
Si wawakili baini, ni mapenzi ya moyoni
-
Jitokeze uwanjani, kikuone hadharani
Karata zimchezoni, kwako huna mshindani
Turufu ividoleni, kubwa khofu yako nini?
Itupe ujiamini, ushashinda si utani
Sayed Al Mugheiry
KIMEPOTEA MACHONI
Date: 28 September, 2004
- Kitandawili kipevu, kukitanzuwa vigumu
Usiwe huo ni wivu, matunda yake ni pummu
Jaribu kuwa mwerevu, penye raha pana sumu
Kuwa wewe mtulivu, subira kweli ni ngumu.
- Utafutacho hakipo, usiku kwako mchana
Uvumao ni upepo, wafananisha wa jana
Hebu mchunguze popo, nyendo zake zina maana
Chunguza kwanza ulipo, huku wakusanya zana.
- Aloiba msichana, wala hatowapa wana
Kama kwake kina mana, atakienzi mnana
Usikae unadhana, mtafute kwa adhana
Tulia huku wabana, huo ndio uugwana.
Hashil S. Hashil
KIMEPOTEA MACHONI
Date: 28 September, 2004
- Changamoto umepewa, ipokee tafadhali
Turufu yako kutowa, afadhaike afeli
Uweze kumkongowa, abwetuke kidhalili
Halijawa sokomoko, lihifadhi chozi lako.
- Ngoma yataka matao, werevu si ujahili
Sawa patasi na mbao, kung'arishana wawili
Mbona ekushinda bao, akakutoka wa pili?
Halijawa sokomoko, lihifadhi chozi lako.
- Maheri Bwana pulika, jina lako litasibu
Dagaa hapewi paka, kulinda ni masaibu
Mwenyewe hukuyataka? kukusaliti muhibu?
Halijawa sokomoko, lihifadhi chozi lako.
Ahmed Rashid.
|