.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Kwakheri Ramadhani

Related links

Kwakheri Ramadhani

Date: 11 November, 2004

  1. Namshukuru Manani, kwa zake nyingi rehema,
    Kauleta Ramadhani, mwezi ulio na huruma,
    Atujalie imani, tushikamane daima,
    Kwaheri wende salama, karibu tena mwakani.

  2. Karibu tena mwakani, kwaheri wende salama,
    Yale tuloyatamani, tuyashike hima hima,
    Yatufae duniani, na kesho huko kiama,
    Kwaheri wende salama, karibu tena mwakani.

  3. Tuyashike kwa yakini, yale tuliyoyasoma,
    Athari iwe moyoni, mwili usende mrama,
    Tutaingia motoni, na huku tunalalama,
    Kwaheri wende salama, karibu tena mwakani.

  4. Tuidumishe amani, maisha yawe salama,
    Wabara na visiwani, sote ndugu Islama,
    Tutende ya ihsani, tuyaache ya dhahama,
    Kwaheri wende salama, karibu tena mwakani.

  5. Swaumu ya Ramadhani, walifunga toka zama,
    Wa huko Uarabuni, pia bandari salama,
    Ikafika vijijini, hadi Unguja na Pemba,
    kwaheri wende salama, karibu tena mwakani.

  6. Kukesha Misikitini, kwa safu wamesimama,
    Wakiomba Yamanani, atupe istikama,
    Tujeingia peponi, waume kwa wanamama,
    Kwaheri wende salama, karibu tena mwakani.

  7. Tufate ya Ramadhani, maadili yalo mema,
    Uislamu ndio dini, ubishi tuweke nyuma,
    Tukiacha ya Qur’ani, tutaila michongoma,
    Kwaheri wende salama, karibu tena mwakani.

  8. Beti nane kituoni, kalamu imesimama,
    Namuomba Rahamani, atupe zake karama,
    Tuisimamishe dini, iende bila kukwama,
    Kwaheri wende salama, karibu tena mwakani.

Eye Witness

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet