|
|
Laiti Siwele Nyuni!
Date: 12 March 2004
- Laiti ! siwele nyuni, haruka haja uliko
Tukangia faraghani, hapungua sikitiko
Hakupa yangu lisani, nawe ukanipa yako
Natamani kuya kwako, lakini sina idhini
- Dalili ya kutamani, nawe waifahamia
Uningizile moyoni, siwezi kuvumilia
Ndipo hafanya huzuni, shughuli ikaningia
Kwako natamani kuya, lakini sina idhini
Muyaka Bin Haji Al Ghassany
Limeletwa Zanzinet na Maher Fundi
Laiti Siwele Nyuni!
Date: 13 March 2004
- Ulitakalo wafanya, halihitaji idhini
Fanya kama panya, kutafuna kwa imani
Wala usione haya, mapenzi yatakulani
Mahaba yanahikaya, hukufanya hamkani.
- Mapenzi sumu ya nyoka, yakikupamba hutoki
Mndu utaita choka, furusadi shokishoki
Akiitaka talaka, machozi tabu kutoka
Lakufanya kwenda Makka, huenda ukaokoka.
- Mengi tunayatamani, kuyapata si rahisi
Leo wawa nyani, kesho wageuka ngisi
Ulimwengu mtihani, si wengi wanaopasi
Walobaki ni kulani, nakutwangana risasi.
Hashil S. Hashil
Laiti Siwele Nyuni!
Date: 13 March 2004
- Idhini simali kitu, mapenzi sumu katili
Haraka njoo kwetu, kwa nini wakaa mbali?
Hapa kwetu ni kwetu tu, ni lazima ukujali
Njoo nakwita njoo, Njoo nakutamani.
- Idhini uisemayo, sidhani kama dharura
Idhini uitakayo, ni nani aloipora?
Idhini niijuayo, unayo tena ni bora
Njoo nakwita njoo, Njoo nakutamani.
- Laiti utaamua, kuja kwetu japo mara
Moyoni nitapungua, majonzi yanonikera
Kusita kwako tambua, moyoni waniparura
Njoo nakwita njoo, njoo nakutamani
- Njoo nakwita njoo, mwenzako nnaumia
Usinitenge, njoo, wabaya wanirandia
Unaibiwa, njoo, kwa haraka kimbilia
Idhini wacha, njoo, njoo nakutamani
Mohammed Omar
Laiti Siwele Nyuni!
Date: 14 March 2004
- Siko mbali ni njiani, ni njiani nnakuja
Nakuja bila idhini, nione ulo yataja
Ulotaja hadharani, ndio kubwa yangu haja
Ingawaje siamini, lakini kwako nakuja
- Umenijaza tamaa, na hamu ya kukuona
Shauku imenivaa, siwezi kungoja sana
Kwangu ishatimu saa, subira sinayo tena
Nnatamani kupaa, niruke tuje kutana
Maher
Laiti Siwele Nyuni!
Date: 16 March 2004
- Lau kama huamini, kwanini ukathubutu
Unatarajia nini, kama hujajidhubutu
Hujalazimishwa sini, uje unifuate kwetu
Ndoo wangu mwandani, moyo umeota kutu
- Ndoo kwa kuridhia, ndipo nitafurahika
Sio kunisumbulia, kwa vile uliniweka
Sasa hebu angalia, waja wasije kucheka
Ndoo japo chungulia, moyo upate pozeka
- Idhini nani atowe, wakati tulishabana
Nilikuwa mimi nawe, ahadi tulopeana
Tukakamatana ndewe, muhali kupoteana
Ndoo usichelewe, utimize uungwana
Said Paul
Laiti Siwele Nyuni!
Date: 16 March 2004
- Kujaribu si makosa, kosa pale kirudia
Nami siviwezi visa, sifanyi kukusudia
Lakini unanitesa, hujuwi, nnakwambia
Ndipo haomba ruhusa, na hali kukulilia
- Mara ngapi mekuomba, na miguu kukushika
Ukaniona naimba, kila nnalo tamka
Ukawa unanitimba, wanifanyia dhihaka
Ulivyo kinitirimba, si sahau nakumbuka
- Moyo hauna pengine, uko kwako umependa
Hauja ona mwengine, ambaye amekushinda
Kwa uzuri si jengine, wanimaliza nakonda
Nnakuja nikuone, na woga sije nitenda
Maher
Laiti Siwele Nyuni!
Date: 16 March 2004
- Ukweli umeusema, kosa kurudia kosa
Sitayarudia tena, makosa na kukutesa
Shahidi wangu Rabana, nimebadilika sasa
Njoo sifanye visa, yaliyopita si ndwele
- Ni dhahiri nilonena, utani meweka kando
Nawe utakujaona, nadharia na vitendo
Mapenzi yalo mwanana, si yale yenye vishindo
Njoo ewe kijana, njoo ujionee
- Mapenzi ni pande mbili, ikiwa munapendana
Mapenzi si ukatili, wala si kukomowana
Mapenzi ni kukukubali, mazuri kutendeana
Njoo sifanye khiana, njoo sikae mbali
- Na mimi ni kama wewe, jinsi nnavyokupenda
Wala sina mwenginewe, awezae kukushinda
Njoo sinisumbuwe, silali, sili, nakonda
Njoo sifanye inda, njoo usichelewe.
Mohammed Omar
Laiti Siwele Nyuni!
Date: 17 March 2004
- Hukuondoshwa na miye, hapo ulipoondoka
Wemfuata apitaye, mimi ukanitoroka
Yanini nikuzuiye, na hali ushanichoka
Haona nivumiliye, wema utaukumbuka
- Madhila yanifika, nikalitafuta tanga
Waja wenisusuika, nikakihama kiunga
Kila pembe neisaka, nayatafuta maganga
Kidogo ningelifika, kuwatukana wakunga
- Wako moyo niuenzi, tusahau yalopita
Uje niujaze penzi, la utamu wa kashata
Ila usifunge tanzi, ni rahisi kulivuta
Funga fundo la hirizi, liwe gumu kukeketa
- Njoo kifua mbele, bado nakuhitajiya
Uchome kama mshale, ardhini ulongiya
Yaliyopita si ndwele, muhimu yalobakiya
Tupendane kwa milele, na tusafiane niya
Said Paul
Kutoka kwa Muyaka bin Hajia: Ushukuru!
Date: 28 March 2004
- Namshukuru Karima, ndiyo hali ya duniya
Kiumbe hupata mema, mawi yakamwondokeya
Kaongezewa rehema, milele kumshukiya
Nami yamenifikiya, kupata hivi si haba
- Nami yamenifikiya, sina nisilofahamu
Mashaka yalonijiya, yali mazito magumu
M'ngu kaniondoleya, mwishowe hatabasamu
Namshukuru Karima, kupata hivi si haba
Tafsiri yake: SHUKURANI
- Namshukuru Sattari, Mola asiye shirika
Mtu hupata mazuri, maovu yakamwepuka
Akaongezewa kheri, kwa miyaka na mikaka
Na mimi yamenifika, nilichopata si tembe
- Na mimi yamenifika, sina nisiloelewa
Mashaka yalonitweka, si mapesi kutukuwa
Mwisho nilifurahika, kwa M'ngu kuyaondowa
Namshukuru Moliwa, nilichopata si tembe
Maher
|