.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Metanzwa na Kiswahili

Related links

Metanzwa na Kiswahili

Date:  02 June 2004

  1. Yanitatiza tatiza, lugha yetu Kiswahili
    Maneno kukaza kaza, kurudia mara mbili
    Silabi kujaza jaza, na kuonyesha kejeli
    Metanzwa na Kiswahili, mwenzenu nisaidieni
  2. Mifano ninayo mingi, ya maneno mara teni
    Naanza na rangi rangi, neno hili sio geni
    Angalia na shangingi, mnipe yenu maoni
    Metanzwa na Kiswahili, mwenzenu nisaidieni
  3. Nakupa na omba omba, uzidi kutafakari
    Kuna kujikomba komba, si jambo la ufahari
    Kwa nini zije sambamba, silabi zilovinjari
    Metanzwa na Kiswahili, mwenzenu nisaidieni
  4. Kuchochota si kuwasha, nakutaka ufahamu
    Kuchachata na kuosha, vyalingana ki-isimu
    Kukeketa, kutonesha, vyaweza kutoa damu
    Metanzwa na Kiswahili, mwenzenu nisaidieni
  5. Kupita pita kwa inda, vijumbani tachukiza
    Kusita sita kutenda, ni ishara ya kuviza
    Kukokota sio kwenda, ni sawa na kuburuza
    Metanzwa na Kiswahili, mwenzenu nisaidieni
  6. Mifano niliyoronga, itizame kwa mapana
    Sio ninaunga unga, ithibiti yangu dhana
    Lugha hii na kutunga, ni vitu vya kufanana
    Metanzwa na Kiswahili, mwenzenu nisaidieni
  7. Yako maneno asili, sauti zinalingana
    Ni mengi sio kalili, hutumiwa kwa bayana
    Ya awali na ya pili, silabi huongozana
    Metanzwa na Kiswahili, mwenzenu nisaidieni
  8. Gugusa ni moja wapo, linanipa wasiwasi
    Dodosa nipe michapo, ukiipata nafasi
    Papasa bado niwapo, nakusanya karatasi
    Metanzwa na Kiswahili, mwenzenu nisaidieni
  9. Naomba unidhukuru, msaada wa sarufi
    Vipi neno msururu, lizirudie herufi
    Na pia neno chururu, silabi zapiga kofi
    Metanzwa na Kiswahili, mwenzenu nisaidieni
  10. Usidhani nahariri, maneno ya maradufu
    Ni mkubwa utiriri, orodha yangu ni ndefu
    Si rahisi kukariri, bila kupata uchofu
    Metanzwa na Kiswahili, mwenzenu nisaidieni
  11. Ninaitua kalamu, nimefikia tamati
    Lakini ninayo hamu, kuzipata zenu beti
    Nipeni yenu matamu, msifanye ati ati
    Metanzwa na Kiswahili, mwenzenu nisaidieni

Kassim O. Ali

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet