|
|
Msiyoyajuwa!
Date: 2 June 2004
-
Mengi yanasimuliwa, juu yangu na mwandani
Watu wataka kujuwa, mecheza turufu gani
Naona mwajisumbuwa, hilo haliwezekani
Wenyewe tumeamuwa, ni siri yetu moyoni
- Yanini kujisumbuwa, nyinyi yawakhusu nini?
Katu hamtoaguwa, mutabakia kudhani
Yeye amenichaguwa, kwake sina mpinzani
Namimi nimeridhiwa, nimezama siutani
- Moyoni memchukuwa, kanijaa akilini
Anang,ara kama juwa, lililopo utosini
Haku wakumpikuwa, na mwenyewe kabaini
Munapita kwenye guwa, tumeshavuna zamani
- Ni bure mutapagawa, sisi hatuwezekani
Hata mukijihashuwa, ndani yetu hamuoni
Sisi tumejaaliwa, kwa uwezo wa manani
Mchele hauna chuwa, sasa mwadondowa nini?
Chakupewa
Msiyoyajuwa!
Date: 3 June 2004
- Ewe uloghaibani, salamu menifikia
Umewapoza mwandani, siri waifatilia
Niwajibu jibu gani, nyoyo zao kutulia
Hii siri ya moyoni, kwa vipi nitawambia
- Nibora ungeimeza, wakabaki kuumia
Sasa umewachokoza, wawatangisha nanjia
Kwani wanibembeleza, nipate kuwafunilia
Kwa kipi kilokupoza, moyoni ukanitia
- Kwako nimesharidhika, sina budi kuwambia
Meniweka mewekeka, nyonda kunitimizia
Wabaki kuhangaika, kwa dhana zilowangia
Siri nimeifutika, nyondani kuifungia
- Kaditamati mefika, sina la kuwaambia
Nakunja wangu mkeka, kitanda nakimbilia
Nnamuomba rabuka, sitoke wakulingia
Wapite kuhangaika, nasie tumetulia
Miminae
|