|
|
MTUKUFU RAMADHANI
Date: 14 October, 2004
- Bismillahi naanza, kwa jina lake muweza,
Nilo nayo kueleza, mupate kuyasikia,
Ya muhimu kuwajuza, na ya kheri kuyajua,
Karibu mgeni wetu, mtukufu Ramadhani.
- Mtukufu Ramadhani, sasa kishatufikia,
Tumjue kwa makini, kuwa ni kujizuia,
Kutia kitu kinywani, na maasi yote pia,
Karibu mgeni wetu, mtukufu Ramadhani.
- Tufunge kwa lengo lake, ucha Mungu kufikia,
Pia umuhimu wake, tupate kuutambua,
Tuzipate radhi zake, kwa kutekeleza Twaa,
Karibu mgeni wetu, mtukufu Ramadhani.
- Mwezi huu Qur'an, ndio imetushukia,
Kafaradhisha Manani, kwa watu kujifungia,
Nguzo zake kwa yakini, nia na kujizuia,
Karibu mgeni wetu, mtukufu Ramadhani.
- Nia kila Isilamu, moyoni kukusudia,
Kujizuia muhimu, alfajiri sawia,
Hadi jioni kutimu, bila ya kuingilia,
Karibu mgeni wetu, mtukufu Ramadhani.
- Katika yaliyo Sunna, ni kufuturu mapema,
Na daku usiku sana, na Qur'an kusoma,
Na kuwa karibu sana, na kwa swala kusimama,
Karibu mgeni wetu, mtukufu Ramadhani.
- Kufanya mema muhimu, na miezi ilosalia,
Kwa kutafuta elimu, na swala kujiswalia,
Zaka na hija kutimu, kila ovu kuondoa,
Karibu mgeni wetu, mtukufu Ramadhani.
- Kama unalazimika, mwezi ukiusikia,
Ufunge bila mashaka, hadi siku kutimia,
Viwanjani kufurika, Iddi kwenda jiswalia,
Karibu mgeni wetu, mtukufu Ramadhani.
EYE WITNESS
|