|
|
Date: 22 November, 2004
Nimelipenda sana shairi hili kwa kitu kimoja: beti ya mwisho imekusanya maudhui yote ya
beti tatu za mwanzo kwa ustadi mkubwa sana! Hapa ndipo, chambilecho
waingereza, wanapotafautishwa, "boys from men"!
Hili shairi ni zito kama nanga ya meli! Mtindo huu sijapata kuuona kwenye
mashairi yote niliyowahi kuyasoma. Na ujue kuwa nimeshasoma mashairi
mengi sana! Mtindo huu wa kuandikwa beti kama chane za ukili - ubeti mmoja
mmoja, kwa maudhui yake - kisha zikapakaswa chane hizo zikaingia zote
kwenye ubeti (ukili) mmoja wa mwisho, hakika umenifurahisha sana!
Hassan Omar Ali
Dallas.
NATAMANI
- Madamu maji mtoni , Daima yachuruzika
Hata na ije tufani , Mwishowe huburudika
Mto kwa kujiamini , Kwa pozi huteremka
Na pendo langu jamani , Hasha halitanyambuka
Mto kaukausheni , Ndiyo pendo takauka
- Madamu bustanini , Mauwa yanachanuka
Jua na mvuwa si shani , Mauwa yatachipuka
Vipepeo kitaluni , Haweshi kurukaruka
Na pendo langu juweni , Muhali kupukutika
Bustani zivunjeni , Ndiyo pendo tavunjika
- Madamu nyota angani , Kote zimechawanyika
Hata lije wingu gani , Mwisho wingu huondoka
Nyota hubaki makini , Huzidi kunawirika
Na pendo langu yakini , Katu halitotoweka
Nyota kaziangusheni , Ndiyo pendo taanguka
- Nikupendae moyoni , Powa usitie shaka
Kwenye mto ukingoni , Nakusubiri kufika
Twende kwenye bustani , Pendo lizidi pambika
Na huku nyota mbinguni , Sisi zinatumurika
Natamani natamani , Siku ifike haraka
KIITIKIO
Nikupendae moyoni , Powa usitie shaka
Natamani natamani , Siku ifike haraka
Shairi : Saleh M. Barkey
|