|
|
NIMLE VIPI SAMAKI
Date: 22 November, 2004
- Nawauliza malenga, ninyi mlio bobea,
Magwiji kutoka Tanga, na hata wa kule Pemba,
Unguja Mbeya Igunga, swali ninawatolea,
Nimle vipi samaki, samaki anayenuka?
- Nimempata Mwaloni, ni pale Mwanza sokoni,
Ninaye hapa jikoni, mwenzenu ninabaini,
Ninayo njaa tumboni, samaki namtamani,
Nimle vipi samaki, samaki anayenuka?
- Magamba nimeparua, namwandaa samaki,
Na tumbo nikatumbua, nikapata taharuki,
Hewa akaichafua, nikapigwa tahamaki,
Nimle vipi samaki, samaki anayenuka?
- Njaa miya inauma, moyo konde nikapiga,
Ndipo mimi nikasema, nitaandaa mafiga,
Na nitampika vyema, nikaondoa uwoga,
Nimle vipi samaki, samaki anayenuka?
- Limao nikanyunyiza, saumu na pilipili,
Nikadhani nimeweza, samaki kumkabili,
Nimewazoea pweza, hawahitaji shubili,
Nimle vipi samaki, samaki anayenuka?
- Wala sikufua dafu, juhudi hazikufaa,
Na ilizidi harufu, pote ilitapakaa,
Imezidi maradufu, nimebaki kushangaa,
Nimle vipi samaki, samaki anayenuka?
- Nimejipikia wali, na uko kwenye sinia,
Naandaa maakuli, samaki namhofia,
Dua zangu nikasali, na uma nitatumia,
Nimle vipi samaki, samaki anayenuka?
- Nikamleta kinywani, harufu ikazidia,
Amenishinda jamani, miye ninawakiria,
Nifanye nini jamani, samaki nilopikia,
Nimle vipi samaki, samaki anayenuka?
- Kijijini wanicheka, na wengine wamenuna,
Na hamu imenitoka, njaa bado ninaona,
Kipande kimedondoka, miye simtaki tena,
Nimle vipi samaki, samaki anayenuka?
- Ninacho kichefuchefu, naweka mbali sahani,
Imenishinda harufu, ya samaki wa Mwaloni,
Sasa nimejawa hofu, samaki siwatamani,
Nimle vipi samaki, samaki anayenuka?
Shairi la Mwanakijiji
Limeletwa na Walii Genderi.
|