.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Nini Kosa Langu?

 

Related links

NINI KOSA LANGU ?

Date: 14 July, 2004


  1. Ewe uliye mwandani, salam yangu pokeya
    Nisikize kwa makini, moyo kunisabiliya
    Nataka wako undani, upate nisaidiya


  2. Tumetokana zamani, hasidi wakiumiya
    Ukinipa ya moyoni, na thamani kunitiya
    Kimekugeuza nini, mara menigeukiya


  3. Kosa langu kitu gani, kheri kunitamkiya
    Usipite vipembeni, lana kunipakaziya
    Alokamilika nani, katika hii duniya


  4. Haitakuwa vibaya, iwapo utanambiya
    Kama nimekukoseya, ni radhi kukwangukiya
    Wala sitoona haya, kwako wewe mardhiya

MIMINAE

NINI KOSA LANGU ?

Date: 18 July, 2004

  1. Mwendani sinishtaki, Likupatalo nyamaza
    Mimi sitokushiriki, wala sitokuuliza
    Kula mtupa tariki, hawachi kujipoteza
    Asietaka kufunzwa, hasalimilki na jambo.


  2. Nalikwambia kitambo, mwendani wangu sikiza
    Sicheze na Mawi mambo, ukanambia tacheza
    Leo twapigana kumbo, kula twendapo husoza
    Asietaka kufunzwa, hasalimiki na jambo.


  3. Ulijifanya mwekevu, kula jambo waliweza
    Kwa kutamania nguvu, akili ukapoteza
    Leo yamekua wavu, tatizi mekutatiza
    Asietaka kufunzwa, hasalimiki na jambo.


  4. Nalikwambia latisha, ukapinga tangu mbele
    Na leo limekutwesha, vumilia vile vile
    Mwiba wa kujitonesha, mtu haambiwi pole
    Asonyooka milele, hasalimiki na jambo.


  5. Undani wangu ni huo, nao sio mwegineo
    Nimekujulisha hayo, kurekebisha ni kwako
    Dunia si tegemeo, huzamisha wenye vyao.
    Asietaka kufunzwa, hasalimiki na jambo.

Abdul

 

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet