|
|
Nipo!
Date: 17 May 2004
-
Nipo papo si baidi, nayachunza yapitayo
Nipo pangu meshtaudi, nafahamu mufanyayo
Nipo sijenda mradi, nasikia munenayo
Ningalipo sijauka
- Ningalipo sijauka, sina pa kuelekeya
Naapa sijaondoka, hili ni letu pamoya
Wala msitie shaka, sambamba twaelekeya
Hadi nanga kuitia
- Hadi nanga kuitia, mikono tutashikana
Hakuna la kunitoa, japokuwa twabanana
Japo kwa kuchechemea, hatua mbele mwanana
Najuwa nimechelewa
- Najuwa nimechelewa, ela kufika lazima
Msiniwache wazawa, kwa vile nilisimama
Ilibidi kuyagawa, maji yalizidi pima
pumzi zilinishia
Mbarouk (Mnyonge wa Nyali)
|