|
|
NJOO BABA KARUME
Date: 9 November, 2004
-
Miaka imetimia , Leo minne kutimu
Sote tumefurahia , Hakika yako awamu
Nyoyo zina asalia , Unatutoja utamu
Muda tumefurahia , Uloishika hatamu
Umma uko furahani , Arba sanaa kutimia
Njoo tena mwakani , Kura tutakutilia
-
Muda umekwenda kasi , Kufumba na kufumbua
Hapakuwa wasiwasi , Mambo yamekuonyokea
Hapakungia utesi , Sera zimetimilia
Umekaa kwa wepesi , Raia twafurahia
Umma uko furahani , Arba sanaa kutimia
Njoo tena mwakani , Kura tutakulitilia
-
Shida umezimaliza , Uchumi meunyanyua
Mishahara hukusaza , Bei zikadidimia
Uhalifu umeviza , Nje tunajilalia
Maji yametumaliza , Kunywa na kuogelea
Umma uko furahani , Arba sanaa kutimu
Njoo tena mwakani , Kura tutakulitilia
-
Chekwa madawa hakika , Nani wa kuzusha hoja
Maradhi kuatilika , Hilo hakika faraja
Mchana mlo wafika , Hapo Mnazimmoja
Ole wao tawafika , Kwetu walio wakuja
Umma uko furahani , Arba sanaa kutimu
Njoo tena mwakani , Kura tutakutilia
-
Nani ataeuliza , Huyo macho hana tena
Barabara zachagiza , Kwa hilo umekazana
Mabanda wayamaliza , Skuli wajaza zana
Ajira umezikaza , Ufanisi wafanana
Umma uko furahani , Arba sanaa kutimu
Njoo tena mwakani , Kura tutakutilia
-
Rushwa umeisokota , Tenda wazitangazia
Mirija umeikata , Madeni wasawazia
Tunajua hutosita , Mbuga wachanjagia
Nguvu kwetu utapata , Mitano kuongezea
Umma uko furahani , Arba sanaa kutimu
Njoo tena mwakani , Kura tutakutilia
-
Kidete umesimama , Chama una kipa somo
Na umoja kama chuma , Wayadonoa makomo
Atokupinga twasema , Tutamtia matomo
Simama baba simama, Tukakusinge kwa somo
Umma uko furahani , Arba sanaa kutimu
Njoo tena mwakani , Kura tutakutilia
-
Wewe hakika ni moto , wapinzani kuchomea
Ni mrengo wa kushoto, Sera kuzisimamia
Hakika simba mtoto , Hakuna kwako sawia
Cha thamani chetu kito , Tayari kukitetea
Umma uko furahani, Arba sanaa kutimu
Njoo tena mwakani Kura tutakulitilia
Ally Saleh
|