.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

RABI TWEPUSHE NA NARI

Related links

RABI TWEPUSHE NA NARI

Date: 04 November, 2004

  1. Hamdu za Maulana, Muumba janna na nari
    Wokovu Ya Rabbana, maasi yamekithiri
    Viumbe twatafunana, kimetuzidi kiburi.
    Yatuaga Ramadhani, Rabbi twepushe na Nari.

  2. Kumi la mwisho mwungwana, jiweke mbali na shari
    Ya shetani mwenye lana, asi wa Allah Qahari
    Atujia kwa mapana, kuzishawishi suduri
    Yatuaga Ramadhani, Rabbi twepushe na nari.

  3. Tutiye moyo dhamiri, tusijifanye hodari
    Jahanamu kali nari, huwakumba majabari
    Huchoma na kuadhiri, wakosefu makafiri
    Yatuaga Ramadhani, Rabbi twepushe na nari.

  4. Saumu ituathiri,tutubu dhambi tukiri
    Wanojitia ghururi, Haawiya yawasubiri
    Watachomwa matajiri, wa inda wenye viburi
    Yatuaga Ramadhani, Rabbi twepushe na nari.

  5. Nyoyo zikose sururi, kuasi si ufakhari
    Pokea langu shauri, sijitie ujabari
    Mja ngia tahayuri, hakuna jambo la siri
    Yatuaga Ramadhani, Rabbi twepushe na nari.

  6. Mwenzangu ngia nadhari, utende lilo la kheri
    Tambua Mola Qahari, yuko nawe huna siri
    Alijua la dhahiri, na la batini vizuri
    Yatuaga Ramadhani, Rabbi twepushe na nari.

  7. Jahanamu yavinjari, yawangoja majeuri
    Na wale wasofikiri, wapenda umashuhuri
    Wala hawangii ari, kurejea kwa Ghafuri
    Yatuaga Ramadhani, Rabbi twepushe na nari.

  8. Wakiasi hawajali, wapenda sifa titiri
    Nyoyo kama majabali, kamwe hazingii nuri
    Hawasimami kusali, wamwasi Allah dhahiri
    Yatuaga Ramadhani, Rabbi twepushe na nari.

  9. Nakhatimisha qauli, kiyama siku hatari
    Funga ziwe maqubuli, hiyo siku ya hashiri
    Twakuomba ya Jalali, Ya Alimu ya Jabbari
    Yatuaga Ramadhani, Rabbi twepushe na nari.

Ahmed Rashid.

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet