.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Yuwaja Mgeni Wetu

 

Related links

YUWAJA MGENI WETU

Date: 28 September, 2004

  1. Ya Allahu ya Karimu, Rahimu ya Rahmani
    Ya Rabi Mola Adhimu, hamdu zako Manani
    Amani kwa muadhamu, Rasuli wa tumaini
    Yuwaja mgeni wetu, kipenzi chetu azizi.

  2. Naikumbusha qaumu, habibu yuko njiani
    Ni johari mahashumu, waridi la busitani
    Fakhari ya Isilamu, dhahabu tuitunzeni
    Yuwaja mgeni wetu kipenzi chetu azizi.

  3. Wekuja musitaqimu, wajumbewe barazani
    Kuitangaza saumu, Rajabu na Shaabani
    Tukawaona ni sumu, ujinga metuzaini
    Yuwaja mgeni wetu, kipenzi chetu azizi.

  4. Tujiandae muamu, kukaribisha mgeni
    Tujongee kwa Rahimu, kwa tahajudi nyumbani
    Tujipambe kwa saumu, na sala misikitini
    Yuwaja mgeni wetu, kipenzi chetu azizi.

  5. Tusingoje baragumu, tukajajuta usoni
    Qiyama siku ni ngumu, liqau kwa Rahmani
    Anza sije jilaumu, kesho kesho hadi lini
    Yuwaja mgeni wetu, kipenzi chetu azizi.

  6. Inawirishe kaumu, msifika Ramadhani
    Twakusubiri kwa hamu, pingu atiwe shetani
    Fika baki humu humu, siende twakutamani
    Yuwaja mgeni wetu, kipenzi chetu azizi.

  7. Sabau kwa hii zamu, beti chache nabaini
    Ramadhani tufahamu, tu wageni wa Manani
    Vipi tumekosa hamu, hatufungi Shaabani?
    Yuwaja mgeni wetu, kipenzi chetu azizi.

Ahmed Rashid.

 

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet