|
|
Ameumbwa Malkiya
Date: 25 July 2005
-
Karibu ya yangu macho, mbele kanisimamiya
Na kila alicho nacho, kamili kimetimiya
Amira hana kificho, peke yake malkiya
-
Dunia ameumbiwa, aiamuru ni yake
Na taji alilopewa, halina mfano wake
Kichwani katunukiwa, vito vyote pambo lake
-
Vingi visivyo idadi, vinashindana kung'ara
Almasi zumaridi, kama nyota zake sura
Yakuti zabarijadi, zimeshikana imara
-
Yake shingo menyo'oka, dede imemsimama
Kifua kisicho shaka, kimemnyanyuka wima
Kimwana ameumbika, huchoki kumtazama
-
Uso umemkunjuka, amejawa na bashasha
Anakenya mkicheka, jambo la kufurahisha
Hasa panapo dhihaka, na meno hukuonesha
-
Mungu kampa kipawa, hadhi yake kumuona
Kwa uzuri alopewa, hamna wa kufanana
Mrembo wa kushtuwa, mtoto bado kijana
Maher ( Unique )
|