.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Bofulo Siri Nataka

 

 

 

 

 

 

Related links

Bofulo Siri Nataka

Date:  8 October, 2005

  1. Bofulo nimekumbuka, nimekumbuka nyumbani
    Na mengi yalotendeka, na visa vya bekarini
    Visa vya wenye kuoka, na walaji taireni
    Nauliza nijuvyeni, bofulo siri nataka

  2. Wapi utamu watoka, mwenzenu mimi sioni
    Nijuvyeni si dhihaka, na siri ya mtumbwini
    Vipi unga kupondeka, kwa kuchovywa miguuni
    Nauliza nijuvyeni, bofulo siri nataka

  3. Toka dakhari na kaka, bofulo ipo nchini
    Imedumu kwa miaka, mehimili ushindani
    Meliwa na kila rika, asubuhi na jioni
    Nauliza nijuvyeni, bofulo siri nataka

  4. Na huko tulikotoka, mkate huu wa shani
    Ilikuwa ni mashaka, kuutia mkononi
    Wengi tukisononeka, kuukosa majumbani
    Nauliza nijuvyeni, bofulo siri nataka

  5. Kama wewe si kikaka, utakaa msongoni
    Hata mbele ukifika, hutaamini machoni
    Mikate 'memalizika, haya sasa ondokeni
    Nauliza nijuvyeni, bofulo siri nataka

  6. Songambele na shirika, Furaha ya Visiwani
    Namna gani mwapika, mikate hii jamani
    Jee ni kweli hakika, ufundi si wa wageni?
    Nauliza nijuvyeni, bofulo siri nataka

Kassim O. Ali

Bofulo Siri Nataka

Date:  10 October, 2005

  1. Kunena sifa ya mja, vitendo vya muungwana
    Mti shina ndio haja, bila ringi gari huna
    "Boya" ndio maharaja, kinyume bofulo huna
    Kahani kuambizana, siri bado haijaja.

  2. Diriki kuni korija, na tanuri la aina
    Uwe fundi wa vioja, uliyepevukiana
    "Boya" ndio lenye haja, Si hivyo uanze tena
    Tujuvye tukijuvyana, siri bado haijaja.

  3. Unga bora wa kutaja, uwe nao wa aina
    Na mafuta ya kufuja, na ya nazi za kukuna
    "Boya" vibaya likija, safari ianze tena,
    Tuambe kiambiana, siri bado haiaja.
  4. Siri bado kuitaja, Wala si kwayo hiyana
    Mbili si moja na moja, wa mangungu wajuwana
    Mkwijini si kuvuja, Fomula never kuona
    Siri bofulo wanena, ni ya mafundi kangaja.
Omar Fakih, Gwangju (RoK).

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet