.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Chakupewa Tukumbuke

 

 

 

 

 

 

Related links

Chakupewa Tukumbuke

Date:  27 May 2005

    Ewe bwana Chakupewa, uko wapi mepoteya
    Mwaka sasa umekuwa, tangu nime kusikiya
    Au huko umepewa, mambo yame kunogeya
    Ukenda hata kutowa, kwaheri ukatwambiya

Unique

Chakupewa Tukumbuke

Date:  27 May 2005

    Enenda kote wendako, jongoo, jiti situpe
    Angalia utokako, Chakupewa ni kweupe
    Sienende koko hoko, jicholo nasi utupe
    Wenzako usitutupe, tukumbuke wenzi wako

Ahmed Rashid

Chakupewa Tukumbuke

Date:  27 May 2005

    Halahala Chakupewa, haifai kukimbia
    Pengine umezidiwa, na mambo ya kidunia
    Na katu haitokuwa, we kazi kukuishia
    Mugwana usitutupe, tukumbuke wenzi wako

M. Simba

Chakupewa Tukumbuke

Date:  27 May 2005

    Wenzio wakuthamini, ujijue cheo chako
    Unajifichia nini, ukatukhini wenzako
    Hebu rudi uwanjani, lipunguze hilo deko
    Nakuasa situtupe, tukumbuke wenzi wako

Saleh Barkey

Chakupewa Tukumbuke

Date:  28 May 2005

  1. Ujumbe niloupata, hauna dowa hakika
    Siku nyingi zimepita, Namimi sikusikika
    Sikuwa kwenye matata, Kwalo nimenusurika
    Ningeweza hata nyata , Kwa hilo nahuzunika

  2. Kwaheri sikuitowa , kwa vilebado sijenda
    Mambo yalinichukuwa , muda wangu ulikonda
    Kila hijipapatuwa , seyafika hata kenda
    Vizuri kunishtuwa , Na huko ndiko kupenda

  3. Ahsante Ikhwani , hakika nyinyi wakweli
    Nitarudi uwanjani , zaidi kwa kulahali
    Wallahi nakutamani , Niwaone mafahali
    Mumenitia thamani , Sidhani nastahili.

Chakupewa

Chakupewa Tukumbuke

Date:  28 May 2005

  1. Tulihuzunika sana, kututoka uwanjani
    Tukawa twaambizana, mwenzetu kafikwa nini
    Kahama bila kunena, akatwacha tumbioni
    Kwa upande wangu sina, memaliza mitaani

  2. Wa Rashidi Ahmedi, henenda na mbio zake
    Salehe akashtadi, tuhimu tuhangaike
    Ili upate kurudi, uwanja uchangamke
    Tukawa twabisha hodi, kila mlango na wake

  3. Hakuna tuliyo acha, nyumba tulizimaliza
    Yetu khofu mejificha, kuona twakuchagiza
    Ndugu zako wakachacha, na uvumba kufukiza
    Juu ya wetu mbacha, mpaka mengia kiza

  4. Leo tumefurahika, mwenzetu umechomoza
    Ndugu yetu umefika, ya dhiki ume yapoza
    Tulikuwa tumechoka, moyo ikituunguza
    Kuona umeondoka, na kubaki tukiwaza

Unique

Chakupewa Tukumbuke

Date:  28 May 2005

  1. Kweli tulihuzunika, zama liponyerereka
    Muhibu tulikusaka, pori, msitu na nyika
    Yuko wapi mtajika, Chakupewa msifika
    Tenda utalolitenda, usitutupe wenzako

  2. Kama yakikupalia, mate lipokitamka
    Ila tukisimulia, mwenza wapi katoweka
    Vyano vilituishia, ruhani hakuzumbuka
    Tenda utalolitenda, usitutupe wenzako

  3. Mahiri hongera Bwana, kutoa nyoka pangoni
    Hata kilima ngenena, Chakupewa mhisani
    Roho zingetulizana, ungezuka muangani
    Tenda utalolitenda, usitutupe wenzako

Ahmed Rashid

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet