|
|
NYUKI
Date: 11 September, 2005
Shairi hili la NYUKI nililetewa na Sk. Khamis bin Nassor Al-Nabhani Mola amrehemu kabla ya kufariki kwake. Ameeleza kua mtungaji wa shairi hili ambae ni mshairi wa enzi zake za zamani hakutaka jina lijulikane na wengi na ndio maana hakulieneza kwa watu wengi. Kabla kufariki kwake Sheikh Khamis, Mola amrehemu, alisema ndio maana hivi sasa katika kisiwa cha Pemba utalikuta shairi hili kwa watu wawili nao ni yeye mwenyewe na Sarhan bin Matar.
- Mambo ya juzi Selemu, Amma hayawasifiki
Hicho ni kisa adhimu, Wala mwerevu hacheki
Waarabu mahashumu, Vidudu kuwahiliki
Kumbe kukimbia nyuki, Mashekhe mbio ni bora
- Vita vya nyuki vigumu, Nakhiyari vya bunduki
Waja hawana salamu, Wala hawanasihiki
Wakitokea karamu, Kataani hailiki
Kumbe kukimbia nyuki, Mashekhe mbio ni bora
- Tulitaraji wageni, Saa mbili hawazuki
Wote wako mibiyeni, Wanazama kama diki
Baadhi ya ariyani, Libasi haziwaviki
Kumbe kukimbia nyuki, Mashekhe mbio ni bora
- Walinipita kikundi, Shekhe Salimu na Muki
Wakaingia kwa fundi, Kilango hakisinduki
Wakaumwaga mtindi, Na majungu ya samaki
Kumbe kukimbia nyuki, Mashekhe mbio ni bora
- Na qadhi bwana Nasoro, Musemae hashituki
Akipata uchochoro, Uchanja haualiki
Alienea michoro, Kwa mashimo na masiki
Kumbe kukimbia nyuki, Mashekhe mbio ni bora
- L-akhi bin Majidi, Musemae hakunjuki
Ajidai majuhudi, Enda kwa punda hashuki
Dharura ikimbidi, Enda mbio hashindiki
Kumbe kukimbia nyuki, Mashekhe mbio ni bora
- Bwana wa Kizuiyani, Mwajuwa simdhihaki
Ejitupia majani, Wala hayamfuniki
Nilimkuta njiani, Unaziba muiliki
Kumbe kukimbia nyuki, Mashekhe mbio ni bora
- Aidha bwana wa Tungwe, Ni mrembo haondoki
Leo pakilia n'gongwe, Kataa hapamueki
Alitambaa na bonde, Hadi rasi ya pichiki
Kumbe kukimbia nyuki, Mashekhe mbio ni bora
- Vilikutana vipungo, Kupungwa bwana Lemki
Nyuki kaipa mgongo, Wala hakutaharuki
Na vile kutoa shingo, Akenda kama hataki
Kumbe kukimbia nyuki, Mashekhe mbio ni bora
- Tamma bin Ibrahimu, Kila epiga falaki
Esema hayatadumu, Efanya kama hataki
Ilishtadi zihamu, Pasiwe alamsiki
Kumbe kukimbia nyuki, Mashekhe mbi ni bora
Limetwa na Saleh Barkey
|