|
|
Kuna Siku Yatakwisha
Date: 11 December, 2005
- Mungu atupe subira, na nyingi stahmala
Itushukie nusura, wahizike zao hila
Iwangie khofu mara, iwatoke kwa ghafula
Kama ndoto walo lala
- Yana tutia uchungu, kila mara tukiona
Kupigwa watu virungu, hata sababu hapana
Wanatugawa mafungu, kwa chuki zisizo mana
Kwa hili hamtapona
- Huku kutu dhalilisha, nako kuna mwisho wake
Kuna siku yatakwisha, yaondoke yende zake
Hawatodumu maisha, Mungu ana siri yake
Tusubiri tusichoke
- Wangapi wameondoka, wameiaga dunia
Walio wakidhihaka, majumba kutuvunjia
Wakapita wakicheka, mabaya kufurahia
Hawapo wamejifia
- Hapa palipo bakia, padogo simbali tena
Muhimu kuvumilia, machungu tunayoona
Tuwe shujaa wa nia! , pamoja kushikamana
Tuangaze mbele sana
Maher ( Unique )
Kuna Siku Yatakwisha
Date: 12 December, 2005
- Usemayo nawafiki, yatakwisha masahibu
Masahibu na mikiki, kuteswa bila sababu
Sababu kudai haki, kudai bila harubu
Harubu si mwendo wetu
- Yatakwisha ya dhuluma, na watu kuadhibiwa
Kuadhibiwa kwa chama, wengi walokichaguwa
Walokichaguwa vyema, sio kulazimishiwa
Kulazimishiwa na wasio wetu
- Watu sasa wamechoka, na matumizi ya dola
Dola ilojipachika, kwa mabavu kutawala
Kutawala kwa shabuka, na majeshi wasolala
Wasolala kwa hofu ya umoja wetu
- Matumizi ya mabavu, ndio kubwa yao ngao
Ngao yetu utulivu, hatujali nguvu zao
Zao nguvu za uovu, hazilindi roho zao
Roho zao, mjuzi ni Mola wetu
- Kubwa wanaloliweza, ni kuchelewesha siku
Siku ya Mola muweza, alopanga tuwapiku
Tuwapiku kuongoza, hakuna mtafaruku
Mtafaruku wa nani kiongozi wetu
Kassim O. Ali
|