|
|
Kukimbia Nyuki
Date: 30 November, 2005
- Asadi etuhiliki, Kwenda tukumbusha leo
Mbona wengine hataki, Afanya mapendeleo
Au ni mtu wa chuki, Ataja watu kwa vyeo?
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Pee na Mchina Tambi, Na huyu hukumtaja
Makumba etoka Bambi,Alojifunga mkaja
Ekuja siku za kambi, Kudondoa moja moja
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Asadi usisahau, Au wajikurupusha?
Na ikiwa ni dharau, Neepo nakukumbusha
Hiyo siku ya pilau, Ndama tulipoangusha
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Kama malenga njoo, Tena takupa na noti
Mustafa Abdoo, Fundi dereva wa boti
Echota wali kwa ndoo, Na Athumani makoti
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Alokabidhiwa supu, Sulemani Mkojani
Hawi mikono mitupu,, Eujaza pakachani
Ana watoto gurupu, Wamngojea nyumbani
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Ee Moh'd Khamisi, Mugheri washindwa kazi
Wajidai udadisi, Kwenda wasema wazazi
Wabakia mufilisi, Kutaja wote huwezi
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Basi nitakutajia, Tena mmoja mmoja
Wa mwanzo aloingia, Buda Baniani koja
Na mbeba sufuria, Kijasho Kinamtoja
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Akaja na babu yangu , Ati enda na wenziwe
Alonambia mwanangu, Selemu leo ingiwe
Tuache bodo na changu, Msi mwana lake jiwe
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Wamjuwa Koti nje, Au hujamsikia
Bwana akipenda punje, Nyali akifuatia
Ni karibu azionje, Nyuki wakamrukia
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Na kina mama kaumu, Wengi walihudhuria
Kirongozi Bisaumu, Ama huyu twakambia
Euna kama sumu, Wali akaukimbia
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Na mwalimu wa sukuli, Alokuja na mwanawe
Alimpiga chuchuli, Kamwambia usinawe
Hawa si nyuki ni nduli, Wataka roho watwawe
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Nikifika thinashara, Aghlabu siongezi
Mana sina mshahara, Na wala hii si kazi
Lakini leo tan'gara, Japo nikose mchuzi
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Ni mambo ya mwaka huu, Na wala hayatajiki
Nakumbuka Mabuluu, Ni mkali hafikiki
Al-Bahri yu juu, Kipangani "Si riziki”
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Kibwanga chesalimika, Si mtu wa kuokota
Alikuwa yu Msuka, Ana gari akokota
Naye angekaza shuka, Kwa tumbo kumsokota
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Na Awadhi Mshihiri, Ee jamani ni mambo
Afadhali kumsiri, Ndiye fundi wa mitambo
Wanzake walikithiri, Walimfanya ni chambo
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Huyu tulikwishajua, Kuwa yeye nuksani
Ee auza halua, Anunue kitu gani
Ni kuwa zimpungua, Wakutiwa gerezani
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Ama Amuri wa Konde, Gando si kwao asili
Aliyakata mabonde, Tena kwa dakika mbili
Wacha matope aponde, Udhani hana akili
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Mapicha asiye hoja, Mtu wa Majimbikani
Ni bado kujikongoja, Ati yeye ni jirani
Asema kwanza angoja, Pilau ije nyumbani
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Kabwera bado mdogo, Na tena anachechea
Kazi kuchoma muhogo, Na nguru kutoela
Pahala palipo zogo, Asema hakuzoea
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Latubi wake usugu, Ekataa kukimbia
Mtu huyu hana ndugu , Pemba na Unguja pia
Yeye ajifanya njugu, Alijivika gunia
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Chumbuni na Pakashume, Hata Mdabi wa Bule
Walijifanya vidume, Lazima wali waule
Basi wache wangurume, Nyuki wapata tungule
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Chani etoka Limbani, Na bakora mkononi
Epita njia za ndani, Hakupitia sokoni
Basi efika Pandani, Njia ya kwao haoni
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Najuta kukulaumu, Mana ni wengi siweshi
Kule kufanya ugumu, Ni bure hatuchokeshi
Kumbe viumbe wagumu, Asonacho hakopeshi
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Sasa nisifu karamu, Wali ulivyopikika
Na nyama ilivyo tamu , Ukigusa yamezeka
Kwa samli kemkemu, Yatoja ikianguka
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Tonge bila ya mpango, Usitafune wameza
Machaza na machinyango, Sio muengo wa pweza
Kutwa uwazi mlango, Bwana Issa etuweza
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Ela wawapi walaji , Wote washapiga mbio
Baki kuponea maji, Hapakupikwa vijio
Betri hazina chaji, Lala usage sikio
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
Kutoka gazeti la Istiqama, mtungaji hajulikani
Limetwa na Suleiman Al Abdely
|