|
|
Kukimbia Nyuki
Date: 02 December, 2005
- Hazikuwa tungo zangu, zangu hazina vihere
Nalalama kwa uchungu, Salehe hewe taire
usitutwange mizungu, ukanivisha shemere
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Yalotokea Selemu, yalihanikiza Wete
Nyuki walifata tamu, ilosongwa na Mapete
Yeye ni watakarimu, wa akidi na wa fete
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Mahiri kawa kidumu, asema asolijuwa
Kasikia kwa mwalimu, Saidi wa Madaniwa
Pariwala yu wa damu , kwa pilau utapowa
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Wakafika wahudumu, kwa austini ya chani
Wakazidi pata hamu, walotokea Limbani
Likapigwa baragumu, bondeni na Kipangani
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Bwana Juma wa Junguni, akaja kapanda punda
Na mpwawe wa Shebani, na wakweze wa Kidunda
Wamepania kwa kani , kusafi yaliyovunda
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Likaingiya gurupu, warabu wa Mkanjuni
Hawa wazijua supu, na lozi za maruhani
Hatoki mtu patupu, pamefikwa shughulini
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Bado viroja vimbali, kaja bwana Khalfani
Mshenga wa serikali, na mwamba maarusini
Katu ndoa si kabuli, usipompa saini
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Joshi likahanikiza, kwa maudi na marashi
Rubuni wakaekeza, kwa vazi la wanawashi
Miwani-mdogo raza, ndie alieshawishi
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Kanga za chapa kipanga, ndizo sare za arusi
Palisadifu malenga, waloghani yasotusi
Hakuna alojitenga, siku hiyo mahususi
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Walipopanda sahari, wanafunzi wa sharifu
Wanotawala membari, za maulidi na dufu
Wazoefu wa viriri, kwa kasida usikhofu
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Ndipo tulipokisia, kuwa ya kale nadhifu
Kwani yaliashiria, kwenye safu ya machifu
Maami walotulia, mashekhe waadilifu
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Kina Sudi wa Mponda, na Abedi Daftari
Shununi wa njia panda, na Yasini Daktari
Hapo mambo yaliwanda, Pilau wakasubiri
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Mara kiwingu chatanda, si cha maji ni cha shari
Wadudu walipotanda , hawesubiri bukhuri
Waliyawacha matunda, na utamu wa sukari
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Vilivamiwa vilemba, kwenye safu mukhtari
Mashekhe waliovimba, kwa elimu za akheri
Nyuki waliwasirimba, kheri ikazaa shari
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Tulistirika sisi, tulovaa suruali
Wakatekwa waasisii, ukapotea muhali
Hapakuwa na jinsi, mbio ni mustakabali
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
- Mahiri kasimlia, bila hata ya kujali
Mengi aloyasikia, hakufumba kwa mithali
Wengine twayachukia, waungwana kawafeli
Kweli Kukimbia Nyuki, Mashekhe Mbio ni Bora
Sultan Ahmed
|