.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Mtukufu Ramadhani

 

 

 

 

 

 

Related links

Mtukufu Ramadhani

Date:  19 September, 2005

  1. Kwa jina lako Rahimu, naanza kusimuliya
    Mola wetu Mkarimu, Ya Rabi nijaaliya
    Nikadiri kukhitimu, haya nalokusudiya
    Niusifu mwezi mwema, mtukufu Ramadhani

  2. Rabi peleka salamu, zende kwa wetu Nabiya
    Mtume wetu Adhimu, Muhamadi Hashimiya
    Na Swahaba Akiramu, na Isilamu jamiya
    Niusifu mwezi mwema, mtukufu Ramadhani

  3. Ya Rabi tupe mwafaka, tufunge bila udhiya
    Saumu yenye baraka, kwako twaitaradhiya
    Tuifunge huno mwaka, na mwakani kwa afiya
    Tuufunge mwezi mwema, mtukufu Ramadhani

  4. Karibu wetu mgeni, kwa hamu twakungojeya
    Ulotukuka yakini, nuru ulivyo eneya
    Mtukufu Ramadhani , karibu twakupokeya
    Kongo mwezi wetu mwema, mtukufu Ramadhani

  5. Mtakatifu adhimu, sote twakukongoweya
    Mwezi uliye muhimu, Mola met’utunukiya
    Twafurahi Isilamu, kila pembe ya duniya
    Kongo mwezi wetu mwema, mtukufu Ramadhani

  6. Mtukufu mwezi mwema , wa sisi kunyenyekeya
    Mwenye kuyatenda mema , bila ya kufanya ri’ya
    Tamswamehe Karima , madhambi kumfutiya
    Kongo mwezi wetu mwema , mtukufu Ramadhani

  7. Mwezi wa nyingi faida , metukuzwa na Jaliya
    Mwezi mwema wa Ibada , na imani kutungiya
    Huondoka zote shida , nafusi zikatuliya
    Kongo mwezi wetu mwema , mtukufu Ramadhani

  8. Mwezi huno wa maana , ameusifu Nabiya
    Ni bora wajulikana , kwa kheri nyingi kungiya
    Mwezi wa neema sana , baraka hutushukiya
    Kongo mwezi wetu mwema , mtukufu Ramadhani

  9. Mwezi mwema wa swiyamu , wa mema kujichumiya
    Milango ya Jahanamu , Rahimu huifungiya
    Na ya Janatu Naimu , wazi hutufunguliya
    Kongo mwezi wetu mwema , mtukufu Ramadhani

  10. Ni mwezi wa Quraani , mwanzo kuteremkiya
    Alipokuja pangoni , Jibirili kwa Nabiya
    Ilikiuwa Ramadhani , wah’ayi alipokeya
    Kongo mwezi wetu mwema , mtukufu Ramadhani

  11. Mashetani makafiri , wawi wa kuharibiya
    Hawawezi kuathiri , wasiwasi kututiya
    Huwafungia Qahari , mbali wakatokomeya
    Kongo mwezi wetu mwema , mtukufu Ramadhani

  12. Imo Lelatil Qad’ri , usiku huo kungiya
    Bora sana mashuhuri , kuliko elifu moya
    Miezi inayo jiri , ya taqwimu Hijiriya
    Kongo mwezi wetu mwema , mtukufu Ramadhani

  13. Na hushuka Malaika , mbinguni wakatokeya
    Kwa amri ya Rabuka , duniyani kufikiya
    Amani hunawirika , hadi swabahi kungiya
    Kongo mwezi wetu mwema , mtukufu Ramadhani

  14. Usiku mwema kipita , wakati huo kungiya
    Na ukija kukukuta , Ibadani umengiya
    Hakika utaipata , Rehema yake Jaliya
    Kongo mwezi wetu mwema , mtukufu Ramadhani

  15. Haya basi Isilamu , mgeni ashaingiya
    Natutimize saumu , tuifungeni kwa niya
    Swala zote tuzikimu , za suna na faridhiya
    Kongo mwezi wetu mwema , mtukufu Ramadhani

  16. Mashekhe na masharifu , wahimizeni jamiya
    Hima tufungeni safu , Tarawehe kuqimiya
    Tumlekee Raufu , kwa kuomba na kuliya
    Kongo mwezi wetu mwema , mtukufu Ramadhani

  17. Darasani tuhimize , wenzetu kuhudhuriya
    Kwa wakati tufulize , misikitini kungiya
    Mawaidha tusikize , atatujazi Jaliya
    Kongo mwezi wetu mwema, mtukufu Ramadhani

  18. Haya shime muombeni , Mola kumnyenyekeya
    Quraani isomeni , kila siku juz’u moya
    Mukiweza ongezeni , muzidi kukaririya
    Kongo mwezi wetu mwema , mtukufu Ramadhani

  19. Na akhiri nimefika , beti nalokusudiya
    Chache naloziandika , tosha kumi na tisiya
    Namshukuru Rabuka, shairi limetimiya
    La kuswifu mwezi mwema, mtukufu Ramadhani

  20. Amina Rabi Dayani , Dua yetu kubaliya
    Ya Ilahi tuauni, tuepushe na udhiya
    Tuifunge Ramadhani, kwa furaha na afiya
    Twaomba yake neema, mtukufu Ramadhani

Shairi: Bw. Swaleh Suheil Abedi
Limeletwa na Sheikh Muhammad Faraj Salim

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet